Katibu
Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dkt. Said Ally Mohamed amemjulia hali Clement
Jackson manusura wa ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa Kariakoo ambaye ni
mtahiniwa wa Kidato cha Nne 2024 anayepatiwa matibabu katika Taasisi ya Tiba ya
Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI).
Dkt. Mohamed
akiambatana na Balozi Dkt. Salim Othman Hamad, Msaidizi wa Rais
anayeshughulikia masuala ya Siasa, amemjulia hali mwanafunzi huyo wa kidato cha
nne wa Shule ya Sekondari Charambe ya Temeke Jijini Dar es Salaam, jana katika
Taasisi ya MOI.
Dkt. Mohamed
amesema wao kama NECTA watatumia kanuni za Baraza hilo katika kushughulikia
suala lake, na kwamba mwanafunzi huyo hatapoteza haki yake ya mtihani.
"Kuhusu
mtahiniwa huyu, Baraza lina taratibu zake litaandaa taarifa zake na kuchukua
hatua stahiki. Lakini niseme tu, tumefarijika kuona katika mitihani yake ya
wiki ya kwanza ameweza kufanya yote na alikuwa anatarijia kufanya mtihani
tarehe 21 mtihani wa Practical Biology 2B," Amesema Dkt. Mohamed na
kuongezea.
"Ni
mwanafunzi ambaye alikuwa na juhudi na ajali (ajali ya kuporomoka jengo la
ghorofa la Kariakoo) imemkuta, lakini Baraza (NECTA) litampa haki yake kadri
inavyostahiki."
Kwa upande
wake mwanafunzi Clement Jackson manusura wa ajali hiyo, amemshukuru Katibu
Mtendaji wa NECTA kwa kumjulia hali na kumpa pole, na kumuomba kushughulikia
suala lake kwa mujibu wa kanuni za Baraza zinavyoelekeza.
Na. Amani Nsello- MOI


0 Maoni