Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa aliyewahi kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Mstaafu David Bugozi Musuguri alijitolea kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa na amani, usalama na mshikamano pamoja na kuifundisha jamii moyo wa dhati wa kuilinda nchi.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Novemba
4, 2024 Butiama mkoani Mara wakati
akiwasilisha salamu za Serikali kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mazishi ya Jenerali Mstaafu
Musuguri.
“ Katika uhai wa kila mmoja wetu ni jambo gani mtu
atakumbukwa nalo, baba huyu ameacha alama ya uzalendo, kujitoa kwake na kuipenda nchi pia aligeuza
changamoto kuwa fursa. Musugurli alikuwa
mstari wa mbele kuliokoa Taifa lake,
tujiulilize sisi tuliobaki tutaacha alama gani? yeye aliacha ya kulikomboa Taifa letu,” amesema Dkt.
Biteko.
“ Alikuwa kiongozi
aliyetamani amani na alisisitiza hakuna vita iliyo nzuri aliamini nguvu
ya mshikamano na katika kipindi hiki tunachoelekea cha uchaguzi tushikamane,
tushirikiane na kuendelea kufanya amani iwe tunu ya Taifa letu,” amesisitiza
Dkt. Biteko.
Fauka ya hayo, amesema Serikali
itauenzi mchango wake daima na kutaja
baadhi ya heshima alizowahi kupewa ikiwa ni
pamoja na kutunukiwa medali
mbalimbali mfano ya Vita ya Kagera na kuwa Serikali itaendelea kusimamia ujasiri, uzalendo na kuthamini
amani.
Vilevile, ameihimiza famili ya
Jenerali Mstaafu Musuguru kurithisha vizazi vyao mema yake pamoja na kuendeleza
umoja na mshikamano miongoni mwao sambamba na kuwashukuru madaktari wote
waliomtibu wakati akiugua.
Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax wakati akimkaribisha Dkt.
Biteko kuzungumza amesema kuwa Taifa limepoteza hazina na kamwe Jenerali
Musuguri hatasahaulika kwa mema yake yote na kuwa Jeshi litaenzi mchango wake.
Naye, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa
Wananchi wa Tanzania, Jenerali Jacob Mkunda amesema kuwa kifo cha Jenerali
Musuguru ni msiba mkubwa si tu kwa Jeshi bali kwa Tanzania yote kulingana na
mchango wake wa ulinzi alioutoa katika utumishi wa umma kupitia Jeshi la
Wananchi wa Tanzania.
“Alishiriki Vita vya Pili vya Dunia
ambavyo vilimjenga, kumkomaza na kumpa uzoefu mkubwa ambao aliporejea nchini
alitumia kwa ajili ya kujenga nchi yake na kuandaa mipango mbalimbali ya kivita
ambayo nchi yetu ilishiriki ikiwa ni pamoja na vita vya mvamizi Iddi Amini na
vya ukombozi wa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika,” ameeleza Jenerali Mkunda.
Akihubiri wakati wa misa hiyo ya mazishi, Askofu wa Jimbo la
Kanisa Katoliki Musoma, Michael Msonganzila amesema kuwa makundi mbalimbali ya watu yamekusanyika
eneo hilo kwa ajili ya kumuaga Jenerali Mstaafu Musuguri na kuwa wameunganishwa
na Jenerali huyo katika tukio hilo.
“Kilichotukutanisha ni misa ya
kumuombea Musuguri aende kwa safari ya amani kuelekea huko kwa aliyetuumba na
alituumba tumjue, tumpende na tumtumikie na mwishowe twende kwake mbinguni,”
amesema Askofu Msonganzila.
Ameendelea kusema “Kumuombea Jenerali
huyu ni tendo la kiimani, tunaamini Yesu alikufa, akazikwa na kufufuka na pia
tunaamini Mungu atawakutanisha wote waliokwisha fariki na Yesu Kristo.”
Askofu Msonganzila amebainisha kuwa
mkusanyiko mkubwa wa watu unafanya watu watafakari kwa kina juu ya uhai wake na
kuwa Jenerali Musuguri alikuwa mnyenyekevu, shupavu na kuwa alipigana vita vya
haki wakati ambao Nduli Iddi Amin kutoka Uganda alivamia Tanzania mwaka 1978.
Kiongozi Mkuu wa Kabila la Zanaki,
Chifu Japheti Wanzagi amesema kuwa Jenerali Musuguri alikuwa na sifa kadhaa
ikiwemo unyenyekevu na mtu wa aina ya pekee ambaye alimjali na kumthamini na
kusaidia kila mtu.
Mzee huyu hakuwa na ukwasi wa mali bali
utajiri wa utu wema, wengi wetu tulipenda kukaa nae na kuzungumza nae mara kwa
mara. Kwa ujumla tunamshukuru Mzee kwa ukarimu na moyo wake wa kusaidia
wahitaji,” amesema Chifu Wanzagi.
Jenerali mstaafu David Bugozi Musuguri
alizaliwa Januari 4, 1920 kijijini kwake Butiama na kufariki Oktoba 29, 2024
katika hospitali ya rufaa Bugando iliyopo Mwanza.
Alitumikia Jeshi kwa miaka 43 ambapo
alihitimu kozi mbalimbali za Jeshi na kuwa Jenerali mwaka 1985. Aidha, mazishi
yake yaliambatana na upigwaji wa mizinga ya heshima 17.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati
0 Maoni