Zaidi ya wafugaji 100 wa Halmashauri
ya Wilaya ya Arusha wamenufaika na mafunzo ya ufugaji bora wanyuki, uongezaji
thamani mazao ya nyuki, uchakataji wa sumu ya nyuki na uandaaji wa maziwa ya
nyuki (Royal Jelly).
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada
ya Mafunzo hayo yaliyotolewa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania
(TAWIRI) wafugaji hao wameshukuru kujengewa uwezo wa ufugaji nyuki kisasa.
"Tumejifunza namna sekta hii ya
nyuki ilivyo na faida kubwa endapo tutafuga kisasa ikiwa ni pamoja na kuongeza
thamani mazao ya nyuki," ameeleza Bw. Meneja Memuruti Menye.
Naye, Mfugaji Bi. Naatosim Parmandi
amesema mafunzo ya vitendo yamekua na tija sana, wameweza kutembelea na
kushuhudia zoezi la upandishaji na ukaguzi wa mizinga pamoja na uchakataji wa
asali unavyofanyika maabara
"Kabla ya mafunzo nilikuwa
natumia njia za kiasili kuvuna asali ambapo zilikua zikiwaathiri nyuki," amesema
Parmandi.
Mtafiti kutoka TAWIRI Bw. Kipemba
Ntiniwa ameeleza kuwa, nyuki ni fusra katika kujikomboa kiuchumi ambapo ametoa
wito kwa wafugaji waliopata mafunzo kuwa walimu kwa wengine.
"Ili kufuga nyuki kibiashara ni
muhimu kujua aina ya nyuki ili kuwa na makundi imara, nitoe wito mkawe walimu
wa wengine," amesema Ntiniwa.
Mafunzo hayo yamefanyika Makao Makuu
ya TAWIRI Njiro-Arusha ambapo watafiti wa nyuki
wametoa elimu ya ufugaji bora wa nyuki
wakubwa (wadungao) na nyuki
wadogo (wasiodunga), uongezaji thamani mazao yanyuki, utalii wa nyuki, zana za
ufugaji nyuki kwa wafugaji.
0 Maoni