Mbunge wa
Jimbo la Mbeya Mjini na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.
Tulia Ackson, ametoa wito kwa jamii kuzingatia matumizi ya nishati safi na
kuchukua hatua za kutunza mazingira kupitia upandaji wa miti rafiki.
Akizungumza
katika uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti jana, Dkt. Tulia ambaye pia ni Rais
wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), alieleza kuwa lengo ni kupanda miti milioni
mbili ya kivuli inayoweza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kampeni hii,
inayohusisha Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), inalenga kuhamasisha wananchi wa
Mkoa wa Mbeya, na imehusisha upandaji miti katika shule za msingi na sekondari,
huku ikigusa kata 36.
Dkt. Tulia
alisisitiza kuwa, "Hii ni awamu ya pili ya kampeni yetu. Awamu ya kwanza
tulipanda miche ya matunda 8,000, na sasa tumejizatiti kupanda miti ya vivuli
milioni mbili. Tutaendelea kushirikiana na TFS katika juhudi hizi."
Aidha, Dkt.
Tulia aliiomba TFS kutoa miti kwa ajili ya kupanda katika eneo la Mlima
Kawetele, ambalo lina changamoto ya mazao kutostawi.
Alisisitiza
umuhimu wa kufanya utafiti ili kuona ni aina gani ya miti inaweza kustawi
katika eneo hilo, ambayo itaweza kuhudumiwa na kuvunwa kwa muda wa miaka mitatu
hadi mitano.
Kwa upande
wake, Kamishna wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo, alieleza
kuwa kampeni hii ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan
za kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kulinda rasilimali za misitu.
Alisisitiza
kuwa misitu ni muhimu kwa mazingira yetu kwani hutoa kivuli, matunda, mbao, na
kusaidia kulinda viumbe hai na rasilimali ya maji.
"Spika
Dkt. Tulia anafanya kazi kubwa ya kuhamasisha utunzaji wa misitu ya asili na
tunamshukuru kwa juhudi zake katika kuhimiza sheria za uhifadhi wa
mazingira," alisema Prof. Silayo.
Chifu wa
Mkoa wa Mbeya, Rocket Mwansinga, aliongezea kuwa machifu wanayo jukumu muhimu
katika kulinda rasilimali za misitu na kuepuka uharibifu wa mazingira.
Aliwataka
wananchi na viongozi wa kijamii kushirikiana na TFS katika kulinda misitu ya
asili ili kuepuka athari za kupotea kwa rasilimali za maji.
"Tumepewa
amri na serikali kutunza misitu ya asili, na tutaendelea kushirikiana na TFS
kuhakikisha tunazuia waharibifu wanaokata miti ovyo," alisema Chifu
Mwansinga.
Kampeni ya
upandaji miti milioni mbili ni hatua muhimu katika jitihada za Tanzania
kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi, huku ikilenga
kuhakikisha usalama wa mazingira na uendelevu wa rasilimali za misitu
kwa vizazi vijavyo.
0 Maoni