Naibu Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan katika sherehe za uapisho wa Rais wa sita wa Botswana, Mhe.
Gedion Duma Boko.
Katika
uapisho huo uliofanyika jana katika Uwanja wa Taifa wa nchi hiyo, umeshuhudiwa
na mamia ya wananchi wa Botswana na vitongoji vyake wakiwemo marais na viongozi
wa wakuu kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Rais mteule
wa Jamhuri ya Botswana ameapishwa rasmi kuwa Rais wa Sita wa nchi hiyo kwa
kipindi cha miaka mitano ambapo ameahidi kufanya kazi kwa kuzingatia misingi na
sheria za nchi hiyo. Aidha amesema atatekeleza majukumu yake ya kazi
akijielekeza katika kuleta maendeleo na Usatawi wa Nchi na Wananchi wake.
Akihutubia
taifa kwa mara ya kwanza Rais Boko amesema anajivunia taifa lake la Botswana
huku akiongeza kuwa matokeo ya ushindi na wake ni tukio la kihistoria kwake
huku akiwataka wananchi wa Botswana kushikamana na kushirikiana katika kipindi
kipya cha kisiasa ambacho amesema kinaongozwa na amani matumaini na kujijenga
upya kijamii na kiuchumi.
“Tarehe 30
Oktoba tulithubutu kupima demokrasia, amani na utulivu wan chi hii na sasa
najivunia kwamba tumeshinda mtihani kwa ushindi mkubwa” alisema na kuongeza kuwa
matokeo haya yatapimwa usatawi wake katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Amesisitiza
kuwa Botswana ni Jamhuri moja hakuna sababu ya kugawanyika bali umoja na
mshikamano miongoni mwao na kusahau tofauti bali kuendelea kujenga kizazi kipya
chenye matokeo makubwa zaidi ya sasa.
Awali
wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi wa dini katika hafla hiyo,
wameliombea taifa hilo kuwa na umoja na mshikamano huku wakihamasisha msamaha
miongoni mwa viongozi na wananchi wote pamoja na kuomba utendaji uliotukuka kwa
Baraza la Mawaziri ili waweze kufanya kazi kwa kutetea rasilimali za nchi hiyo.
Sherehe hizo
pia zimehudhuriwa na Rais wa Zimbabwe Mhe. Dkt. Emmerson Mnangagwa, Rais wa
Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema, Rais wa Namibia, Mhe. Dkt. Namgolo Mbumba,
Waziri Mkuu wa Eswatini, Mhe. Russell Mmiso Dlamini, Waziri Mkuu wa Afrika
Kusini, Mhe. Ian Khama, Waziri Mkuu wa Msumbiji, Mhe. Adriano Afonso Maleiane,
Jaji Mkuu wa Nchi hiyo, Spika wa Bunge na viongozi wengine waandamizi akiwemo
Rais Mstaafu wa Botswana Mhe. Mokgweetsi Masisi.
Na. Ofisi ya
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni