Mwanaume
mmoja aitwaye Jackson maarufu kama mjomba anasakwa na Jeshi la Polisi mkoa wa
Mwanza kwa tuhuma za mauaji ya binti mwenye umri wa miaka tisa aitwaye Tatu
Khamis Daniel anayedaiwa kuuawa kwa kukabwa shingoni kisha kubakwa na mwili
wake kutelekezwa kwenye jengo ambalo halijakamilika.
Kamanda wa Polisi
mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa amesema tukio hilo limetokea mnamo tarehe
tatu ya mwezi huu majira ya saa mbili usiku wakati Binti huyo Tatu akiwa
anacheza na wenzake ndipo akatokea Jackson maarufu kama mjomba ambae rafiki wa
baba wa binti huyo, akamchukua kwa ahadi ya kwenda naye dukani kumnunulia pipi
ndipo akatoweka nae kusikojulikana.
Kamanda
Mutafungwa amesema hadi ilipofika kesho yake siku ya tarehe nne ya mwezi huu
majira ya saa kumi na mbili na nusu katika Kijiji cha Nabweko wilayani Ukerewe
ulipoonekana mwili uliokuwa umetelekezwa kwenye jengo ambalo halijakamilika
kujengwa na kutambulika kuwa ni mwili wa binti huyo Tatu Khamis Daniel.
Aidha, Kamanda
Mutafungwa amesema mara baada ya mwili wa binti huyo kufanyiwa uchunguzi
ulibainika aliuawa kwa kukabwa shingoni kisha kubakwa na kwamba mwili huo
umekabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya mazishi.
0 Maoni