MWENYEKITI Mpya wa Tume ya Madini, Janet Lekashingo ameahidi kufanya kazi kwa uadilifu, uaminifu na ushirikiano mkubwa na watumishi na wadau wote wa Sekta ya Madini.
Lekashingo
ametoa ahadi hiyo leo Novemba 8, 2024 akiripoti ofisi za Tume ya Madini
zilizopo Kikuyu, jijini Dodoma tayari kuanza majukumu yake mapya baada ya
kuteuliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Oktoba 31, 2024 kuwa Mwenyekiti mpya
wa Kamisheni ya Tume ya Madini akichukua nafasi ya Profesa Indris Kikula ambaye
muda wake umemalizika.
Amesema, Sekta
ya Madini ina nafasi kubwa ya kubadili mtazamo wa nchi, kubadili maisha ya watanzania pia kubadili uchumi wa nchi.
“Hivyo ni
muhimu sisi watumishi wa Tume ya Madini kuhakikisha kwamba tunaangalia mifumo
yetu kama inastahili, kuhakikisha mazingira maeneo ya migodini yanatuzwa,
kuhakikisha jamii inashirikishwa, nimefurahi kusikia wachimbaji wadogo wanapewa
umuhimu unaostahili,”amesema Lekashingo.
Aidha,
amesema amefarijika kurudi Tume ya Madini kama Mwenyekiti wa Kamisheni na
kumshukuru Rais Dkt. Samia kwa kumuamini na kumpa jukumu hilo muhimu la
kuongoza Tume ya Madini.
“Pia
nimshukuru Mheshimiwa Waziri wa Madini Anthony Mavunde, Katibu Mkuu Mhandisi
Yahya Samamba na viongozi wote kwa kuwa nami katika safari hii,”amesema
Lekashingo na kuongeza.
“Wengi
mnafahamu nimepata bahati ya kutumika kama Kamishna wa Tume ya Madini na
ninaelewa madini yana umuhimu mkubwa katika uchumi wetu hivyo ni jukumu letu
kupitia Tume kuhakikisha Wizara inafanya vizuri kutunza mazingira na madini
yananufaisha watanzania na uchumi wa nchi yetu,”amesisitiza.
Awali,
akitoa taarifa ya Tume ya Madini Kaimu Mkurugenzi wa Leseni na Tehama, Mhandisi
Aziza Swedi kwa niaba ya Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi
Ramadhani Lwamo, amesema Tume ya Madini imeendelea kuimarisha ukusanyaji wa
maduhuli yatokanayo na madini ambapo
kiwango cha makusanyo ya maduhuli ya Serikali kilipanda kutoka Shilingi Bilioni
346.275 zilizokusanywa Mwaka 2018/2019 na kufikia Shilingi Bilioni 753.18 Mwaka
2023/2024.
Aidha, amesema
katika Mwaka wa Fedha 2024/2025, Tume ya Madini imepangiwa kukusanya jumla ya
Shilingi Bilioni 999. 998, ambapo hadi
kufikia Oktoba 31, 2024 Tume imefanikiwa
kukusanya jumla ya Shilingi Bilioni 354. 613 sawa na asilimia 35.46 ya lengo la
mwaka. Makusanyo ya mwezi Oktoba ni Shilingi Bilioni 96.724 sawa na asilimia 116.07 ya lengo la mwezi
Oktoba 2024.
Mhandisi
Swedi amesema, mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeimarika na
kufikia asilimia 9.0 Mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 5.1 kwa mwaka 2018.
Aidha, ukuaji wa Sekta ya Madini uliimarika na kufikia asilimia 11.3 kwa Mwaka
2023 ikilinganishwa na asilimia 5.1 Mwaka 2018.



0 Maoni