KAMISHNA wa Uhifadhi wa Wakala wa
Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo, amewataka wananchi na
wadau wa ufugaji nyuki nchini kuchangamkia fursa ya Mkutano wa Dunia wa Ufugaji
wa Nyuki (Apimondia) utakaofanyika mwaka 2027.
Akizungumza katika Nyuki Marathon
iliyofanyika leo Oktoba 26,2024 Jijini Arusha, Prof. Silayo alisisitiza kwamba
ufugaji nyuki si tu ni biashara bali pia unachangia katika ukuzaji wa utalii na
uhif-dhi.
Marathoni hiyo ilihusisha wanariadha
takriban 500 kutoka mataifa mbalimbali, ikiwa na lengo la kuhamasisha ufugaji
wa nyuki na kutangaza umuhimu wa mazingira.
Prof. Dos Santos alisisitiza kuwa
mashindano hayo ya Nyuki marathon ni ya kwanza duniani na mashindano muhimu kwa
afya, ukuwaji wa sekta ya nyuki nchini na duniani sambamba na kujenga mahusiano
mema ya nchi yetu kimataifa kwa sababu yameleta watu wa mataifa mbalimbali kuja
kushiliki mashindano hayo.
"Lakini kwakuwa tunajiandaa kama
sehemu ya kufanyika kwa Kongress ya 50 ya Apimindia 2027 hapa nchini imekuwa
sehenu nzuri sana yakutuma ujumbe kwamba Tanzania tuko tayari, " anasema.
Anaongeza kuwa utunzaji mzuri wa
mazingira unachangia katika uzalishaji wa nyuki, na hivyo kuongeza uchumi wa
jamii. "Nyuki ni mtaji; wanapaswa kutunzwa kwa kutumia mizinga na
mazingira lazima yalindwe," alisema.
David Mukomana, Rais wa Kamati ya
Kanda ya Apimondia kwa Afrika, alisisitiza umuhimu wa tukio hili kama jukwaa la
kuhamasisha ufahamu kuhusu ufugaji nyuki. Alieleza, "Nyuki Marathon ni
hatua muhimu kuelekea mwaka 2027. Tunaweza kujenga ustahimilivu wa jamii
kupitia ufugaji nyuki."
Mukomana alieleza uhusiano wake wa
kibinafsi na tukio hili, akisema, "Nyuki Marathon ni jambo la pekee sana
kwangu. Linawakilisha hatua muhimu kuelekea mwaka 2027, natambua uwepo wa Meya
wa Arusha kama ishara ya kuonyesha utayali wa jiji hili na Tanzania kuelekea kongamano lijalo."
Meya wa Jiji la Arusha, Maximilian
Iranghe, alitangaza mpango wa kugawa mizinga milioni 2, akisisitiza lengo la
kuongeza idadi ya nyuki katika eneo hilo. "Tunataka Arusha iwe na nyuki
wengi; mkutano wa Apimondia utakuwa chachu katika kuleta maendeleo,"
alisema.
Wakati huo huo, Restetuta Lopes
Lazarus, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Woker Bees Africa, aliongeza kwamba mbio
hizo zililenga kuelezea umuhimu wa nyuki kwa maisha ya binadamu, akisisitiza
kwamba asali ni tiba kwa magonjwa mbalimbali.
Marathoni hiyo, iliyopewa kauli mbiu
"Kuelekea Apimondia 2027," ilidhihirisha umuhimu wa ushirikiano wa
ndani na wa kimataifa katika kukuza ufugaji wa nyuki na kulinda mazingira.


0 Maoni