Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile ametoa wito kwa waandishi wa habari nchini kutumia haki yao ya kidemokrasia kujiandikisha na kupiga kura kuchagua viongozi katika ngazi ya serikali za mitaa, vijiji na vitongoji nchini.
Balile ametoa kauli hiyo mara baada ya
kujiandikisha kushiriki katika uchaguzi huo wa Serikali za Mtaa. Amejiandikisha
Mtaa wa Kitunda jijini Dar es Salaam siku ya Jumamosi, Oktoba 12, 2024.
Mwenyekiti huyo wa Jukwaa la Wahariri
amesema waandishi wa habari pamoja na utekelezaji wa majukumu yao wasijisahau
kutimiza haki hiyo ya msingi.
“Mara nyingi tumekuwa tukiripoti mambo
mengi ya wenzetu, lakini sisi wenyewe tumekuwa tukijisahau. Nitoe wito kwa kila
mwandishi wa habari popote alipo kujiandikisha na kujitokeza kupiga kura
kuchagua viongozi katika mitaa yetu,” amesema Balile.
Balile pia amevikumbusha vyombo vya
habari kufanya ufuatiliaji wa zoezi hilo linavyoendelea pamoja na kutoa elimu
ya mara kwa mara kwa wananchi kujitokeza kwa wingi, kwani baadhi wanachanganya
utaratibu wa Uchaguzi Mkuu unaosimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na wa Serikali za Mitaa unaosimamiwa na
TAMISEMI, badhi wakidai kadi ya Mpigakura wanayo tayari.
Zoezi la uandikishaji wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa serikali
za mitaa, vijiji na vitongoji unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu
limezinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu
Hassan siku ya Ijumaa, Oktoba 11, 2024,
jijini Dodoma.
0 Maoni