WAZAZI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka vijana wachangamkie fursa zinazotokana na maendeleo ya teknolojia katika kujipatia kipato na kushiriki kukuza Uchumi wa Taifa.
Amesema kuwa vijana wanapaswa kutumia
mitandao ya kidijitali kutafuta fursa za masoko na upatikanaji wa bidhaa ili
kufanikisha malengo ya kuifanya Tanzania kuwa Taifa lenye maendeleo endelevu
kupitia nguvu ya vijana na teknolojia.
Mhe. Majaliwa amesema hayo jana (Ijumaa,
Oktoba 11, 2024) wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa
uliyofanyika katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza.
“Dunia nzima ya leo inazungumzia
matumizi ya kidijitali na matumizi haya ya kidigitali yanaenda kukabiliana na
changamoto za karne ya 21, pamoja na
kasi kubwa ya maendeleo duniani. Leo hii tunafanya manunuzi mtandaoni na
hata fursa za biashara zinafanyika kidijitali. ”
Amesema kuwa ni ukweli usiopingika
kuwa maendeleo katika sekta ya dijitali yanatoa fursa nyingi kwa vijana ambao
wana nafasi kubwa ya kujiendeleza na kuleta maendeleo ya Taifa kwa kutumia
kikamilifu ubunifu wao kupitia matumizi ya teknolojia mpya.
Ameongeza kuwa ili kufanikisha lengo
la Dira ya Taifa ya Maendeleo na Malengo ya Maendeleo Endelevu, teknolojia za
kidijitali zina nafasi muhimu ambazo kila mmoja anapaswa kuzichangamkia.
“Teknolojia hizi siyo tu zinarahisha shughuli mbalimbali za kila siku katika
maisha yetu, bali pia zinasaidia katika kufanya maamuzi yenye tija kwa kutumia
mifumo mbalimbali ya kidijitali. ”
Pia, Waziri Mkuu amewataka vijana
waendelee kuwa na matumaini na Serikali kwa kuwa imejipanga kuhakikisha
inawafungulia fursa. “Endeleeni kuiunga mkono Serikali yenu kwa namna ambavyo
imekuwa ikifungua milango ya fursa mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya vijana,
endeleeni kuhakikisha mnakuwa karibu na Serikali ili uweze kufikia ndoto yako
kwenye maisha. ”
Kwa Upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete
amewataka vijana watumie vizuri mifumo
ya kidijitali. “Tutumie kwa matumizi mazuri yasiwe yanayoelekeza chuki,
mgawanyo au mpasuko mkubwa katika nchi yetu, tuitumie ili ituwezeshe kufikia
malengo makubwa tuliyonayo”.
Amesema kuwa dunia ya sasa ni ya
Kidijitali ambayo inaitaka jamii kujua kwamba ili uweze kufanya jambo
linalokwenda na kasi ya dunia ya leo ni lazima ujikite katika matumizi ya
kidijitali.
Kwa upande wake Waziri wa Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Tabia Mwita
Maulid amesema kuwa wataendelea kusimamia maelekezo ya viongozi wa kitaifa ili
vijana wawe mstari wa mbele katika
kujiajiri na kuajiriwa na waweze
kuchangia pato la mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
“Lengo letu ni kuhakikisha Tanzania inaendelea
kuwa na vijana productive Barani Afrika na duniani kwa ujumla, kwa kufanya
hivyo tutakuwa tunamuunga mkono Rais Dkt. Samia ya kuendelea kuijenga
Tanzania”.
0 Maoni