Serikali imejidhatiti kutatua
changamoto zinazowakumba vijana balehe kwa kuweka mazingira salama na rafiki
kwa vijana hao kupitia afua mbalimbali zinazowawezesha kufikia malengo yao na
utimilifu wao kwa ujumla.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu,
Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi aneyasema hayo jijini Dodoma wakati
akifungua mkutano wa wadau wanaotekeleza afua za vijana balehe nchini (NAIA)
kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na
Makundi Maalum mkutano unaofanyika kuanzia 31Oktoba hadi Novemba 01 mwaka huu.
Dkt. Yonazi amefafanua kwamba Ajenda
ya Kitaifa ya kuwekeza katika Afya na maendeleo ya vijana balehe nchini iliyozinduliwa
Aprili 17,2021 ilikua na lengo ni kuharakisha utekelezaji wa maeneo ya
kipaumbele vinavyohusu afya na maendeleo ya vijana balehe katika Mikoa 13 yenye
viashiria visivyoridhisha kuhusu afya na maendeleo ya vijana hao nchini.
“Utekelezaji wa Ajenda umejikita
katika nguzo kuu 6 za ambazo ni kuzuia maambukizi ya VVU, kutokomeza mimba za
utotoni, kutokomeza ukatili wa kimwili, kingono na kisaikolojia, kuboresha hali
ya lishe, kuhakikisha wavulana na wasichana wanabaki shule kukamilisha mzunguko
wao wa elimu, na kuwaendeleza vijana katika ujuzi na ufundi ili wapate fursa ya
kujiari na kuajiriwa,” amesema Dkt. Yonazi.
“Kaulimbiu ya mkutano huu inayosema Utatuzi wa
Changamoto za Vijana balehe kwa Taifa imara inachechemua utekelezaji wa ajenda
hii kwa upana wake kwa kuwa ndiyo pekee yenye uwezo wa kukabiliana na
changamoto hizo za vijana kwa sasa hivyo ni matumaini yangu kuwa kupitia
mkutano huu, mtapata fursa ya kujadili kwa undani kuhusu changamoto zinazohusu
vijana balehe kwa kutumia uzoefu wa utekelezaji wa Ajenda hii kwa kipindi cha
miaka mitatu,” amesema Dkt. Yonazi.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju ametambua juhudi za Mashirika ya Kimataifa na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yaliyoanzisha miradi mbalimbali kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Vijana Balehe wanapata huduma rafiki za afya, elimu ya afya ya uzazi na kupata ujuzi na maarifa ya kuwafanya wamudu maisha yao.
“Mafanikio haya hayajaja hivi hivi,
bali ni jitihada kubwa mlizofanya ninyi Wadau wa Maendeleo kwa kushirikiana na
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyeunda Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, hivyo nachukua fursa hii kuwapongeza kwa dhati kwa
ushirikiano huo mlioonesha na kufanikisha malengo ya Ajenda hii,” amesema
Wakili Mpanju.
Kwa niaba ya wadau, Mwakilishi kutoka
Shirika linaloshughulikia masuala ya Watoto (UNICEF), Edgar Lungu ameishukuru
Serikali kwa kuwezesha wadau kuweza kutekeleza afua zao na kuahidi kuendelea
kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuweza kufanikisha kusudio la Serikali
kuwa na taifa lililo na vijana imara na taifa imara.
0 Maoni