Hatimaye mbinu mpya ya kudhibiti
changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu hususani tembo iliyobuniwa na
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA ambayo tayari imeanza
kutumika kuzuia tembo kuleta athari kwa maisha na mali za wananchi waishio wilaya za Same na Mwanga Mkoani Kilimanjaro
imeanza kuonesha mwelekeo wa mafanikio
baada ya wananchi kukiri
kuwasaidia.
Katika nyakati tofauti, wakizungumza
na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari katika ziara iliyofanywa na TAWA
wilaya za Same na Mwanga Oktoba 31, 2024 Mkoani Kilimanjaro wananchi hao
wameishukuru TAWA kwa elimu waliyowapa, umoja na ushirikiano wanaoutoa kwao
katika kukabaliana na changamoto ya tembo jambo ambalo wanakiri limewasaidia
kujilinda dhidi ya madhara yatokanayo na wanyamapori hao na pia kupata mavuno
Kwa wakati.
"Tunashirikiana na watu wa TAWA
vizuri sana na maelekezo wanayotupa kuhusiana na tembo ni mazuri sana, ni kweli
hawa tembo wanasumbua lakini Kwa kushirikiana inawezekana kuwakabiri,"
amesema Karanga Mhina mkazi wa Kijiji cha Kitamri kilichopo Kata ya Stesheni
wilayani Same.
"Tunawashukuru sana hawa TAWA Kwa
kutupa elimu ya kufukuza hawa tembo, zamani sisi tulikuwa hatulimi ila sasa
hivi tunalima lakini pia wametupa vifaa vizuri sana, mabomu baridi ya kufukuza tembo
na sasa hivi tukiwafukuza angalau tunavuna," ameongeza Mhina.
Naye Afisa Uhifadhi wa TAWA kutoka
kituo cha Ruvu Same Yohana Mgalula amesema kutokana na ukubwa wa changamoto ya
wanyamapori wakali na waharibifu hususani tembo inayowakabili wananchi wa
ukanda huo, Mamlaka kwa kushirikiana na taasisi zisizo za kiserikali walikuja
na mbinu ya kuwashirikisha wananchi Kwa kuhamasisha uundwaji wa vikundi jamii
vya ulinzi wa mazao ambavyo anakiri kuwa vimeleta tija na ufanisi Kwa kiwango
kikubwa.
Mgalula amesema baada ya kuunda
vikundi hivyo, Mamlaka ilivipatia elimu ya kujikinga dhidi ya madhara
yanayoweza kusababishwa na wanyamapori hao sambamba na mbinu za kuwafukuza hasa
pale wanapovamia makazi au mashamba yao. Ikiwa ni pamoja na kuwapatia vitendea
kazi ikiwemo vuvuzela, filimbi, tochi zenye mwanga mkali jambo ambalo
limeviwezesha vikundi hivyo kushiriki kwa zaidi ya asilimia 90 kuwadhibiti
wanyamapori hao bila uwepo wa Askari wa TAWA.
Kwa upande wake Afisa Habari wa TAWA
Beatus Maganja amepongeza mwitikio wa wananchi hao kushirikiriana na Serikali katika kukabaliana
na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu na kusisitiza kuwa TAWA
itaongeza kasi ya kuendelea kuwapa elimu pamoja na mbinu mbalimbali za kukabaliana
na wanyamapori hao sambamba na kuwapatia vifaa vitakavyowasaidia katika
utekelezaji wa jukumu hilo.
"TAWA tutaendeleza kasi ya kuwapa
elimu wananchi katika maeneo mbalimbali yenye changamoto ya wanyamapori wakali
na waharibifu nchini, jukumu hili tutalifanya Kwa nguvu kubwa ili kuhakikisha
wananchi wanaendelea kuwa salama," amesema Maganja.
0 Maoni