Tume ya Madini yafanikiwa kuongeza makusanyo ya maduhuli

 

Tume ya Madini imefanikiwa kuongeza makusanyo ya maduhuli kutoka Shilingi Bilioni 624.6 mwaka 2021/2022 hadi kufikia Shilingi Bilioni 753.8 mwaka 2023/2024.

Kaimu Katibu Mtendaji Tume ya Madini Eng. Ramadhani M. Lwamo amesema lengo la Makusanyo kwa mwaka 2024/2025 ni Shilingi Trilioni 1 sawa na wastani wa kukusanya Shilingi Bilioni 83.33 kwa mwezi.

Eng. Lwamo ametoa maelezo hayo leo Dar es Salaam katika kikao na wahariri wa vyombo vya habari cha kuelezea mafanikio ya utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Madini kwa mwaka 2021/2022-2024/2025.

“Katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Septemba, 2024, jumla ya kiasi cha Shilingi Bilioni 257.89 kimekusanywa,” alieleza Eng. Lwamo na kufafanua, “Makusanyo hayo ni sawa na asilimia 103.16 ya lengo kwa kipindi husika, na pia ni sawa na asilimia 25.79 ya lengo la Mwaka 2024/2025.”

Eng. Lwamo pia ameelezea maeneo ya kipaumbele ya tume hiyo kuwa ni kuimarisha usimamizi na udhibiti katika maeneo ya uzalishaji madini; hususan madini ujenzi na viwandani.

Pia, kuimarisha udhibiti wa biashara haramu ya madini, uboreshaji na usimamizi thabiti wa mfumo wa utoaji wa leseni za madini na kuimarisha mazingira ya uwekezaji kwa wadau wa sekta.

Chapisha Maoni

0 Maoni