Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony
Mavunde leo tarehe 24 Oktoba, 2024 amekutaja na kufanya mazungumzo na Balozi wa
Belarus nchini Tanzania, Mheshimiwa Pavel Vziatkin.
Katika mazungumzo hayo, Balozi Pavel
amebainisha kuwa lengo la ziara yake ni kuendelea kuimarisha diplomasia ya
uchumi baina ya Belarus na Tanzania, kuzifahamu zaidi fursa zinazopatikana
katika sekta ya madini nchini Tanzania na kuonesha namna Belarus ilivyopiga
hatua katika teknolojia na utengenezaji wa mitambo imara inayoweza kutumika
katika sekta ya madini.
Akimkaribisha Balozi Pavel, Waziri
Mavunde alieleza kwamba Nchi ya Tanzania imebarikiwa uwepo wa madini ya aina
mbalimbali yakiwemo ya metali, Vito na madini mkakati na kusisitiza kuwa zipo
fursa lukuki ambazo wawezekaji kutoka Belarus wanakaribishwa kuja kuwekeza
katika sekta ya madini nchini.
Alimweleza kuwa, kupitia falsafa ya
Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya
4R iliyoweka msingi wa mazingira mazuri ya uwezekezaji, tumeendelea kupata
wawekezaji wengi nchini na kuwakaribisha wawekezaji kutoka Belarus kuchangamkia
fursa hiyo.
Aidha, Mheshimiwa Mavunde alimweleza
Balozi Pavel kwamba Tanzania imepiga marufuku ya kusafirisha madini ghafi nje
ya nchi, hivyo ni fursa kwa wawekezaji kuanzishwa viwanda vya kuongeza thamani
ya madini hapa nchini.
Vilevile, Waziri Mavunde alibainisha
kuwa Tanzania ina wachimbaji wakubwa wanaotumia teknolojia za kisasa na wadogo
ambao bado wanatumia zana duni, na hivyo kumwomba Balozi Pavel kuangalia
uwezekano wa kuzalisha mashine za bei nafuu ambazo zitarahisha shughuli za
wachimbaji wadogo ambao wameendelea kuwa na mchango mkubwa kwa uchumi wa Taifa
letu.
Kwa upande wa madini mkakati na
muhimu, Waziri Mavunde alionesha kuwa ipo miradi zaidi ya 12 katika hatua za
mwisho ili ianze uzalishaji na kusisitiza itakapoanza itakwenda kuiweka
Tanzania katika ramani ya nchi zenye uzalishaji mkubwa wa madini mkakati na
muhimu Barani Afrika.
Mwisho, Waziri Mavunde alitumia fursa
ya mazungumzo hayo kukaribisha wawekezaji na makampuni mbalimbali kutoka Nchini
Belarus kuja kushiriki Mkutano wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini (TMIC)
unaotaraji kufanyika tarehe 19 hadi 21 Novemba, 2024 Jijini Dar es Salaam na
kusisitiza kuwa itakuwa ni nafasi ya makampuni ya Belarus kufahamu zaidi fursa
zilizopo nchini kwenye sekta ya madini.
0 Maoni