Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ameahidi neema kwa wanakijiji
wa Kijiji cha Mwaboza, Kata ya Moa katika Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, ambao
sasa wataanza kupata malipo kwa utunzaji wa miti aina ya mikoko.
Dkt. Kijaji amesema Rais Samia Suluhu
Hassan amemtuma kuja Tanga kuwaeleza wanakijiji
wa Mwaboza kuhusu kupatiwa malipo yao ya kutunza mikoko na amewahimiza
wasiikate miti hiyo badala yake wapande zaidi mikoko ili wanufaike nayo.
“Hatuhitaji ukate mikoko yako endelea
kupanda natunataka uendelee kupokea pesa kwa mikoko yako kwa maisha yako wewe na
kizazi chako,” alisema Waziri Dkt. Kijaji na kuongeza, “Hiyo ndio kazi ya Mama
(Rais) na ndio maana kanituma nije Tanga niwaambie maneno haya na anawapongeza
kwa kutunza mazingira na sasa pesa inakuja.”
Dkt. Kijaji aliyasema hayo wakati akielezea
faida ya Utunzaji na Uhifadhi wa Mazingira hasa katika upandaji wa miti aina ya
mikoko wakati akiongea na wanakijiji hao jana Oktoba 23, 2024.
FAIDA ZA MIKOKO
-Mikoko inasaidia kupunguza kasi ya
mawimbi makubwa ya bahari ambayo yangeweza kufanya uharibifu katika maeneo ya
pwani mwa bahari.
-Mikoko pia hutoa mazingira mazuri ya
samaki kuzaliana na kukwepa kasi ya mawimbi makali.
-Mikoko inauwezo wa kuhifadhi hewa ya
ukaa (carbondioxide) kutoka angani na kuzalisha oksijeni kupitia kitendo cha
mmea kiitwacho "photosynthesis".
-Mikoko inachuja maji ya chumvi na
kuondoa 90% ya chumvi inayopatikana katika maji ya bahari na kuingia kwenye
mizizi yake.
Katika ziara hiyo pamoja na mambo mengine Dkt. Kijaji alikagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi ya maendeleo na kufanya mikutano ya kuongea na wananchi mkoani humo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akifafanua jambo mara
baada ya kuzindua Shule ya Sekondari Kiomoni iliyopo Kata ya Mzizima,
Halmashaurii ya Jiji la Tanga mkoani Tanga.
0 Maoni