Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji
wa Mitaji ya Umma (PIC) imeipongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)
kwa mafanikio yake katika kutekeleza majukumu yake.
Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti
wa kamati, Mhe. Augustine Vumma Hole, wakati wa semina iliyofanyika leo kwa
ajili ya kuwasilisha mkakati wa TFS katika kuongeza mapato ya Serikali na
kuimarisha uhifadhi.
"Nawapongeza kwa kazi nzuri
mnayofanya, ambapo mmekuwa na mchango wa bilioni 25 kwenye mfuko mkuu wa
Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/24," alisema Mhe. Hole.
Meneja Mipango wa TFS, Bi. Neema
Mbise, alieleza kwamba mapato ya TFS yameendelea kukua, yakifikia bilioni
165.58 kwa mwaka huu.
Aliongeza kuwa, "uwekezaji mkubwa
unaofanywa na Serikali na dhamira ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiyo
sababu kuu ya ukuaji huu na uhifadhi kuimarika."
Kamishna wa Uhifadhi TFS, Prof. Dos
Santos Silayo, alipokea pongezi hizo na kutoa ufafanuzi kuhusu hoja mbalimbali
za wajumbe wa kamati.
Prof. Silayo pia alizungumza kuhusu
mikakati mbalimbali ya TFS, ikiwemo biashara ya kaboni ambayo inatarajiwa
kuleta Dola milioni 65.4 kwa mwaka, kuongeza mapato kupitia utalii wa ikolojia,
na kukuza uzalishaji wa mazao ya misitu na nyuki.
"Katika kipindi cha miaka minne,
Wakala umeweza kukusanya shilingi bilioni 13.1 kutokana na biashara ya utomvu
kutoka mashamba ya miti ya Sao Hill, Buhindi, na Rubya," alisisitiza Prof.
Silayo.
Kwa kumalizia, alieleza kuwa TFS
itaendelea na usimamizi madhubuti na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu
na nyuki, kuhakikisha kwamba maendeleo yanafikiwa bila kuathiri mazingira.
0 Maoni