WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
taasisi yoyote ambayo inahitaji kutwa ardhi ambapo wananchi wanaishi au
wanafanya shughuli mbalimbali za maendeleo lazima iwe imetenga bajeti ya
kuwafidia kabla ya kufanyika kwa zoezi hilo ili kuondoa usumbufu.
Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Oktoba
31, 2024) wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kusini, Ali Kasinge ambaye
alitaka kujua kwa nini Serikali isione uwezekano wa kuruhusu watu waliofanyiwa
tathmini kwa ajili ya kutwali maeneo yao wasiruhusiwe kuyaendeleza wakati
wakisubiri kulipwa fidia.
“Utwaaji huo unapaswa kuzingatia
sheria, nitoe wito kwa taasisi zote ziwe za umma au sekta binafsi pale ambapo
wanafikiria kuanzisha mradi na mradi huo unagusa maeneo ya wananchi ni lazima
wajipange kwanza kibajeti kabla hawajaenda kufanya tathmini ili wanapokwenda
kufanya tathmini ukipata gharama unalipa mara moja na wananchi waweze kupisha
na kwenda eneo lingine.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewaagiza
Makatibu Tawala wa Mikoa na Mabaraza ya madiwani wazifuatilie Halmashauri ili
kuhakikisha zinatenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya
maendeleo kama ilivyoainishwa kwenye mwongozo wa fedha wa sheria ya Serikali za Mitaa inayoelekeza utengwaji
wa fedha zinazopatikana kwenye mapato ya ndani ya halmashauri na kuzitumia
kwenye utekelezaji wa miradi.
Vilevile, Mheshimiwa Majaliwa
ameiagiza Ofisi ya Rais TAMISEMI inapofanya ufuatiliaji ijiridhishe moja kati
ya ajenda ni kufuatilia upelekaji wa fedha za maendeleo zilizotokana na mapato
ya ndani ya halmashauri ili wananchi waweze kupata maendeleo wanayoyahitaji.
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati
akijibu swali la Asia Halamga aliyetaka kujua kauli ya Serikali kuhusu
halmashauri ambazo hazifuati takwa la kisheria la kupeleka asilimia 20 ya
mapato ya ndani katika vijiji kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo.
0 Maoni