Wakala ya Barabara za Vijijini na
Mijini (TARURA) imekamilisha ujenzi wa vivuko na daraja la Mto Mnyamasi lenye
urefu wa mita 20 pamoja na kufungua barabara ya Kambanga-Ifinsi yenye urefu wa
Kilomita 37 inayounganisha vijiji vya Ifinsi, Kambanga na Bugwe vilivyopo kata
ya Tongwe Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi.
Kaimu Meneja wa TARURA Mkoa wa Katavi,
Mhandisi Japhet Bengesi ameishukuru serikali kwa kutoa shilingi Bilioni 1.5 kwa
ajili ya ujenzi wa madaraja na vivuko na kufungua barabara inayoanzia
Kambanga-Ifinsi mpaka Kijiji cha Bugwe ambapo imewezesha wananchi kusafirisha
mazao yao kwa urahisi.
“Kikwazo kikubwa kilikuwa katika mto
Mnyamasi ambalo ni eneo la bonde hapo awali hakukuwa na mawasiliano lakini
kutokana na juhudi za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutuletea fedha,
tumeweza kujenga makalavati ya ukubwa tofauti 7 na barabara unganishi ambapo
imekuwa mkombozi mkubwa maana hili ni eneo kubwa sana la uzalishaji”, alisema.
Naye, Mwenyekiti wa Kitongoji cha
Mnyamasi, Bw. Ngisa Muyanga ametoa pongezi na shukrani kwa serikali kwa
kuwatengenezea barabara hiyo ambayo hapo awali ilikuwa haipitiki, wananchi
walikuwa wanavuka kwa shida kusafirisha bidhaa zao.
“Tulikuwa tunavuka kwenye maji kipindi
cha masika, wakina mama walikuwa wanajifungulia njiani magari yalikuwa hayapiti
na tulikuwa tunashindwa kusafirisha biashara zetu, lakini kwa sasa tunaishukuru
serikali, watu wanavuka kwa urahisi na magari yanapita katika vipindi vyote,”alisema
Bw. Ngisa.
Wakati huo huo Mkazi wa kijiji cha
Ifinsi, Bw. Ibrahimu Temi alisema, kipindi cha nyuma miundombinu ilikuwa tabu
walikuwa wanabeba magunia yenye mazao mabegani kuvuka ng’ambo, lakini sasa
magari yanaingia kijijini na wanakoboa mpunga na kusafirisha mchele kufikisha
Mpanda kwa urahisi.
Kwa upande wake, Bi. Eunice Shola
mkazi wa kijiji cha Ifinsi, ametoa shukrani kwa Rais Samia kupata barabara hiyo
kwani wanawake walikuwa wanapata shida kuvuka na wengine walijifungulia njiani,
sasa hivi hawana shida ya usafiri magari ya wagonjwa yanafika hadi kjijini na
kupeleka wananchi hospitali.
0 Maoni