Tanzania itaendelea kuimarisha misingi
ya uhusiano wa diplomasia baina yake na nchi ya Namibia katika kuimarisha
mahusiano yaliyopo katika nyanja mbalimbali huku mchango wa Tanzania katika
uhuru wa Namibia ukitajwa.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Ummy Nderiananga ameyasema
hayo jana Oktoba 24 alipotembelea Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Namibia,
ambapo aliambatana na watendaji wa ofisi hiyo kwa lengo la kushiki Mkutano wa
Nane wa Ngazi ya Viongozi (High Level Meeting) kuhusu masuala ya kupunguza
athari za maafa pamoja na kikao cha tisa cha Jukwaa la Kanda la Afrika la
kupunguza athari za maafa.
Naibu Waziri Ummy ameeleza kuwa hatua
hiyo imefikiwa kutokana na uongozi makini, na mahiri wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyojipambanua
kidiplomasia na kuhakikisha mahusiano ya Taifa na nchi nyingine unakuwa wenye
manufaa na kuiletea nchi heshima katika nyanja mbalimbali.
“Hakika Tanzania imeendelea kuwa
kitovu cha amani na utulivu, hii imetokana na uongozi mahiri wa Mhe. Rais Dkt.
Samia kwa miongozo na maelekezo yake katika kuhakikisha nchi inaendelea
kujipatia maendeleo,”amesema Mhe. Ummy.
Aidha, katika mazungumzo na mwenyeji
wake ambaye ni Afisa Mambo ya Nje Mkuu na Kaimu Balozi wa Tanzania nchini
Namibia Elias Tamba ameeleza kuwa, nchi ya Tanzania itaendelea kushirikiana na
Namibia katika masuala mbalimbali kwa kuzingatia urafiki uliopo baina ya
Mataifa hayo mawili toka kipindi cha Uhuru wa Namibia ambapo Tanzania inakumbukwa
kwa mchango wake.
Ujumbe wa Tanzania nchini Namibia
umeongozwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri mkuu anayeshughulikia masuala ya
Sera, Bunge na Uratibu Ummy Nderiananga akiwa ameambatana na Timu yake kutoka
Ofisi ya Waziri Mkuu akiwemo Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Dkt. Jim Yonazi,
Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi hiyo Brig. Jenerali Hosea
Ndagala, Mkurugenzi wa Tathmini na Ufuatiliaji Ofisi ya Waziri Mkuu Charles
Msangi, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa ofisi hiyo pamoja na January Kitunsi.


0 Maoni