Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
Tanzania (TAWA) leo Oktoba 24, 2024 katika ukumbi namba 44 jengo dogo la
utawala bungeni Dodoma imewasilisha taarifa ya utendaji wake ya mwaka 2023/24
kwa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii iliyojikita katika
kudadavua majukumu ya kiuhifadhi na utalii katika kipindi husika.
Akiwasilisha taarifa hiyo mbele ya
Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Timotheo Mnzava (Mb) Kwa niaba ya Kamishna wa
uhifadhi wa TAWA, Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi Mlage Kabange amesema katika
kipindi cha mwaka 2024/25, Mamlaka imepanga kukusanya kiasi cha zaidi ya
shilingi billioni 94 ambapo hadi kufikia mwezi Septemba, 2024 Mamlaka
imekusanya zaidi ya shilingi bilioni 23.8 sawa na asilimia 102.96 ya lengo la
robo ya kwanza ya mwaka.
Kuhusu ongezeko la matukio ya
wanyamapori wakali na waharibifu nchini Kabange amesema Wizara imekuja na
mkakati wa kuvuna baadhi ya spishi za wanyamapori hao ili kupunguza athari Kwa
maisha ya wananchi na mali zao ambapo amebainisha kuwa wanyamapori watakaovunwa
ni mamba na viboko katika maeneo mbalimbali nchini yenye changamoto ya wanyama
hao ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vizimba 10.
Sambamba na hilo, Mamlaka itaendeleza
matumizi ya teknolojia ikiwemo kufunga visukuma mawimbi Kwa makundi ya tembo
kwa ajili ya kurahisisha ufuatiliaji na matumizi ya mabomu baridi ambayo
yameonekana kuleta matokeo mazuri kwa maeneo mbalimbali nchini.
Akiongelea suala la utatuzi wa
migogoro ya mipaka, Mlage Kabange amesema Mamlaka imefanikiwa kuweka alama za
mipaka za kudumu (vigingi) 826 katika Mapori ya Akiba manne (4) ambayo ni
Kilombero, Mpanga/Kipengere, Liparamba na Igombe na Pori Tengefu Lunda Nkwambi
hii ikiwa ni baada ya kushirikisha wananchi, Wizara za Ardhi na TAMISEMI na KU
za Mikoa na Wilaya.
Vilevile Mamlaka imefanikiwa kulipa
fidia ya Shilingi millioni 482.57 kwa wananchi wa maeneo ya Kagera, Msumbiji na
Elbebek yaliyopo katika Kijiji cha Kisondoko na eneo la Ndaja katika Kijiji cha
Keikei Wilaya ya Kondoa katika Pori la Akiba Mkungunero ili waweze kuhama ndani
ya hifadhi hiyo ili kupisha shughuli za kiuhifadhi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Timotheo Mnzava
ameipongeza TAWA Kwa kasi ya ukusanyaji maduhuli na kuitaka iongeze kasi ya
kutangaza vitalu vya uwindaji wa kitalii.
Pia, ameiomba Wizara iangalie namna ya
kutatua changamoto ya uhaba/uchache wa watumishi wa TAWA ili kuongeza tija na
ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Na. Beatus Maganja- Dodoma
0 Maoni