Tanzania yapigiwa mfano katika kukabili maafa

 

Serikali ya Tanzania imeendelea kuonesha umahiri wake katika masuala ya menejimenti ya maafa nchini kwa kuzingatia mifumo sahihi ya kukabiliana na maafa na matumizi ya teknolojia ya kisasa pamoja na miongozo, kanuni na sheria mbalimbali zinazoongoza katika uratibu wa maafa hayo.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Ummy Nderiananga wakati akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kuhitimishwa kwa Mkutano wa nane wa ngazi ya viongozi kuhusu masuala ya kupunguza athari za maafa pamoja na Kikao cha tisa cha jukwaa la kanda la Afrika la kupunguza athari za maafa na vilivyofanyika jijini Windhoek nchini Namibia.

Naibu waziri Nderiananga ameeleza kuwa, uwekezaji mkubwa umefanywa na Serikali ya Tanzania hususan katika kuhakikisha teknolojia inavusha Taifa katika kukabili maafa ambapo Serikali ilianzisha Kituo cha Ufuatiliaji wa Mwenendo wa Majanga katika Kituo cha Taifa cha Operesheni na mawasiliano ya dharura nchini Tanzania ambacho kimeifanya nchi kuwa mahiri katika masuala ya menejimenti ya maafa hususan katika kuzuia, kupunguza kujiandaa na kukabili maafa pindi yanapotokea.

Katika hatua nyingine Naibu waziri Nderiananga amezungumzia kuhusu mkakati wa miaka kumi wa Nishati safi ya Kupikia ambao utekelezaji wake umeanza mwaka huu hadi 2034, ameeleza kuwa unalenga kuhifadhi mazingira, kulinda afya kwa kuzuia matumizi ya kuni na mkaa ili kuepuka athari za mabadiliko ya tabia nchi.

“Suala ya mabadiliko ya tabia nchi linaathiriwa na ukataji wa miti inayopelekea uharibifu mkubwa wa mazingira na kuchagiza ukosefu wa mvua za kutosha, uwepo wa ukame unaoathiri uzalishaji wa chakula, tunampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuzindua mkakati huo,”alisema.

Amesema moja ya mikakati ambayo Tanzania imejiwekea ni kuhakikisha zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034

 

"Kama nchi tumejipanga kuhakikisha Taasisi za Serikali na Mashirika binafsi yanawekeza ipasavyo katika matumizi ya nishati safi kwa maslahi mapana ya mazingira safi na salama, Afya zetu na Afrika kwa ujumla, " amesisitiza Mhe. Nderiananga.

Awali akifungua mkutano huo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Kazi na Uchukuzi Nchini Namibia John Mutorwa amesema mikutano hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa ambapo awamu hii imefanyika nchini Namibia na kuwakutanisha wadau zaidi ya elfu moja wa  maafa kwa nchi za Afrika wakiwemo wataalamu kutoka katika ngazi za kitaifa, Serikali za mitaa, Mashirika ya Umoja wa Kitaifa na Kimataifa, Asasi za Kiraia, sekta binafsi, taasisi za elimu na utafiti na wanahabari, na hii imetajwa kuwa ni mafanikio makubwa kwa bara la Afrika.

“Tunashukuru kwa namna nchi zilivyojitokeza kushiriki mikutano hii muhimu katika kuhakikisha masuala ya maafa yanakabiliwa na kuwa na Afrika stahimilivu katika maafa, tunawashukuru sana Mawaziri mlioweza kushiriki mikutano hii, nasi tumepata heshima kama nchi, na tunaahidi kuendelea kuimarisha mashirikiano yetu kama Bara la Afrika,”alisema Mhe. Mutorwa.

Aidha, alitoa rai kwa kila nchi kuona umuhimu wa kujipanga kukabili maafa bila kujali utofauti na hali za Mataifa ya Afrika, lengo kuyafikia na kuyaishi malengo na kuwa tayari kusimamia masuala haya.


Chapisha Maoni

0 Maoni