Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa uhusiano wa Tanzania na Singapore zitaenzi
uhusiano uliopokati yake ambao umedumu kwa muda mrefu, kwa kuainisha sababu za
uhusiano huo na kuongeza ufanyaji wa biashara kati ya nchi hizi mbili.
Dkt. Biteko ameyasema hayo Oktoba 21,
2024 akiwa nchini Singapore mara baada ya kukutana na kufanya mazungunzo na
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Viwanda na Biashara wa Singapore Mhe. Gan Kim
Yong.
“ Tunatakiwa kujifunza kutokana na
uhusiano huu na hasa kutoka Singapore kwa kuwa mmepiga hatua katika sekta ya
nishati hadi kuwa na uwezo wa kufikia mahitaji ya juu ya umeme ya zaidi ya
Gigawati 8, hicho ni kiasi kikubwa ikilinganishwa na Tanzania yenye takribani Megawati 3000 ambapo hadi mwaka
2030 tumepanga kufikia Megawati 10,000,” amesema Dkt. Biteko.
Amesisitiza “Mpango huo hauwezi
kutokea bila kuwa na ushirikiano na wadau na nchi zingine kama Singapore, ni
matumaini yetu kuona ushirikiano huu unaendelea kukua kati ya nchi zetu na
kuleta manufaa kwa wananchi.”
Dkt. Biteko ameipongeza Singapore kwa
uzalishaji wa umeme wa jua na kusema kuwa Tanzania inaendelea na jitihada zake
za kuzalisha umeme huo.
Akitaja miradi ya nishati inayoendelea
kutekelezwa, Dkt. Biteko amesema kuwa kwa sasa nchi inaendelea na utekelezaji
wa mradi Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha megawati 2115.
Aidha, upembuzi yakinifu unaendelea
kuhusu miradi mbalimbali ya uzalishaji umeme.
Fauka ya hayo, Dkt. Biteko amemualika
Naibu Waziri Mkuu wa Singapore, Mhe. Yong nchini Tanzania.
“Kwa niaba ya Serikali na Rais Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan tutafurahi ukija Tanzania na tuna amini kuna maeneo
mengi ya kushirikiana nanyi,” amesema Dkt. Biteko.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu wa
Singapore, Mhe. Yong amesema kuwa nchi yake ipo tayari kuendelea kushirikiana
na Tanzania na kuwa nchi hizo zina mahitaji ya kufanana.
Aidha, amesema kuwa Singapore inatumia
zaidi gesi asilia kama chanzo cha nishati ingawa pia inatumia umeme unaozalishwa
kwa maji, jua na upepo.
Vilevile amesema nchi yake iko tayari
kushirikiana na Tanzania katika kubadilishana uzoefu wa masuala mbalimbali
yanayohusu sekta ya nishati.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati
0 Maoni