Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imepokea vifaa tiba mbalimbali kutoka Africa Future Foundation kwa kushirikiana na Jeju National University Hospital, msaada ambao utasaidia kuendelea kuimarisha na kuboresha huduma za matibabu kwa wagonjwa wanaofika hospitalini hapa.
Vifaa tiba hivyo vitatumika kuendelea
kuboresha huduma za dharura kwa wagonjwa, wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji,
kufuatilia mienendo ya wagonjwa baada ya kufanyiwa upasuaji ili kuhakikisha
afya zao zinaendelea kuimarika kwa wakati.
Akipokea msaada huo, Naibu Mkurugenzi
Mtendaji Dkt. Julieth Magandi ameshukuru kwa msaada huo kwani umekuja wakati
muafaka na pia utaongeza ufanisi katika kutoa huduma na kuwafanya wananchi
kuendelea kupata huduma bora.
Dkt. Magandi ameongeza kuwa Taasisi
kutoka Korea Kusini zimekuwa na ushirikiano wa manufaa makubwa na Muhimbili
Mloganzila kwa kusaidia katika maeneo ya kuwajengea uwezo wataalam, kuleta
wataalam kutoka Korea kwa lengo la kubadilishana uwezo pamoja na kutoa msaada
wa vifaa tiba.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa Africa
Future Foundation Seong Hong amesema taasisi yake kwa kushirikina na Jeju
National University Hospital wataendelea kutoa misaada kwa hospitali hii ili
kuhakikisha Watanzania watapata huduma bora za afya.
Hospitali ya Taifa Muhimbili
Mloganzila imekuwa na ushirikiano wa muda mredu na taasisi za Korea Kusini
ikiwemo Korea Foundation for International Health Care (KOFIH), Africa Future
Foundation (AFF), Vision Care na Jeju National University Hospital.
0 Maoni