Majaliwa: Uwekezaji mkubwa umefanyika Sekta ya Hali ya Hewa

 

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea na jitihada za kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya hali ya hewa nchini ambapo ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, Tanzania itakuwa na Rada saba ikiwa ni kiwango kikubwa cha Rada katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Amesema kuwa hatua hiyo ni mwendelezo Serikali za kufanya uwekezaji katika sekta ya hali ya hewa nchini kwa kufunga miundombinu ya kisasa ya hali hewa ili kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa taarifa za hali ya hewa.

Amesema hayo leo (Jumapili, Oktoba 13, 2024) wakati alipotoa tamko la kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Madhara ya Maafa, Jijini Mwanza.

“Nitumie fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uwekezaji mkubwa katika eneo hili lakini pia kuendelea kutoa kipaumbele kwa makundi maalumu na kuweka mikakati thabiti inayolenga kuwawezesha vijana kiuchumi na kijamii. ”

Amesema kuwa maadhimisho ya mwaka huu yanatoa fursa ya kuimarisha ushirikiano wa kitaifa na kimataifa ili kuunganisha juhudi za kuwalinda watoto na vijana dhidi ya athari za majanga.

“Ili kuifikia adhma hiyo, katika ngazi ya Taifa tunapaswa, pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kuwa tunatumia fursa hii kutoa mafunzo kwa jamii kuhusu mikakati ya kujikinga na maafa, hasa elimu ya hali ya hewa na jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi; kuandaa mikutano ya kujadili changamoto za maafa na kupanga mikakati ya pamoja. ”

Ameongeza kuwa mamlaka husika zinapaswa kuendesha kampeni za uhamasishaji kuhusu umuhimu wa elimu na mawasiliano ya hatari, pamoja na ushiriki wa jamii, kuandaa matukio ya utamaduni na michezo ili kuhamasisha jamii na kutoa elimu kwa njia ya burudani, kuendeleza tafiti kuhusu madhara ya maafa pamoja na  kutoa taarifa kwa umma ili kuongeza uelewa.

Aidha, Waziri Mkuu ameielekeza wizara yenye dhamana ya elimu na taasisi zake kuhakikisha wanaendelea kuimarisha mitaala ya elimu ili ijumuishe masuala ya usalama shuleni, kupunguza hatari, na uelewa wa majanga. “Vilevile, kuhakikisha mafunzo kwa walimu kuhusu mbinu za kufundisha masuala haya kwa wanafunzi yanaendelea kuimarisha. ”

 

Pia,  Mheshimiwa Majaliwa amezitaka mamlaka husika ziendelee kuhamasisha na kuwezesha matumizi ya mbegu zinazokomaa kwa muda mfupi pamoja na utunzaji wa chakula cha binadamu na malisho ya mifumo. “Imarisheni utoaji taaluma ya matumizi ya mbinu za kilimo cha kisasa kinazohitaji maji kidogo. ”

Awali, akipokea taarifa kuhusu maadhimisho ya Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru na Kumbukizi ya Miaka 25 ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere, Mheshimiwa Majaliwa amesema ameridhishwa na hatua za maandalizi ya maadhimisho hayo.

Mgeni Rasmi katika maadhimisho hayo yatakayofanyika katika uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza, Oktoba 14, 2024 atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete amesema kuwa maandalizi yamekamilika ambapo  pamoja na mambo mengine Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia kushiriki katika ibada maalum ya kumuombea Baba wa Taifa itakayofanyika katika Kanisa Katoliki la Parokia ya Mtakatifu Fransisco Xavery Jijini Mwanza.

Chapisha Maoni

0 Maoni