Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Serikali inawakaribisha wawekezaji
katika sekta ya nishati ili kuongeza kasi ya usambazaji, uzalishaji na
unganishwaji wa nishati nchini Tanzania.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Oktoba
21, 2023 nchini Singapore wakati akishiriki mjadala kuhusu nishati akiwa pamoja
na Waziri wa Madini na Nishati kutoka
nchini Cambodia, Mhe. Keo Rottanak na Waziri wa Maliasili kutoka nchini New Zeland Mhe. Shane Jones wakati wa
ufunguzi wa Wiki ya Kimataifa ya Nishati ya nchini Singapore.
“Serikali haziwezi kufanya kila kitu
zenyewe hivyo ni muhimu kushirikiana na sekta binafsi. Sisi Tanzania tunawaalika
sekta binafsi ije kuwekeza katika sekta ya nishati kwa ajili ya kuimarisha
uzalishaji, upatikanaji na usambazaji nishati na kuboresha maisha ya watu kwa
ujumla,” amesema Dkt. Biteko.
Akizungunzia, ajenda ya nishati safi
ya kupikia nchini amesema kuwa ni matokeo ya utafiti uliofanywa na kubaini kuwa
idadi kubwa ya Watanzania wanatumia kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia hali
inayosababisha magonjwa ya mfumo wa upumuaji na uharibifu wa mazingira.
Ili kupunguza athari hizo, Dkt. Biteko
amesema kuwa Serikali imeandaa mkakati unaolenga kuhakikisha Watanzania
asilimia 80 wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
“Serikali imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya
nishati safi ya kupikia pamoja na kuhakikisha nishati safi inapatikana kwa
urahisi na bei nafuu na hivyo tunawakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza katika
hili kwa sababu soko lipo,” amesema Dkt. Biteko.
Kuhusu jitihada za Serikali za kuimarisha sekta ya nishati nchini, Dkt. Biteko ametaja miradi mbalimbali inayofanywa na Serikali ikiwemo mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2115.
“Serikali inaendeleza vyanzo vipya vya
nishati mfano umeme wa jua, upepo na gesi, aidha kwa sasa asilimia 51 ya umeme
unazalishwa kwa maji. Tanzania tumeendelea na maandalizi ya kuziuzia umeme nchi za Kenya, Rwanda, Burundi
na sasa tunaendelea na mradi kwa ajili ya kuunganisha na nchi ya Zambia,
kupitia Umoja wa Mauzio ya Umeme wa pamoja katika nchi za Afrika Mashiriki na
Jumuiya za Kusini mwa Afrika (SADC) tuna soko la uhakika na hivyo
tunawakaribisha wawekezaji kuja kushirikiana nasi,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Naye, Waziri wa Madini na Nishati kutoka
nchini Cambodia, Mhe. Keo Rottanak amesema kuwa mwaka 1998 nchi yake ilifanya
mageuzi makubwa katika sekta ya nishati na kuwa sasa asilimia 99 ya vijiji ina
umeme.
“Tutahakikisha tunafikisha umeme
katika nyumba za watu na malengo yetu ni ifikapo mwaka 2030 umeme unaozalishwa
kwa jua kuwa mbadala wa umeme unaozalishwa na maji, amesema Mhe. Rottanak.
Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili
na kutoka nchini New Zeland, Mhe. Shane
Jones amesema kuwa nchi yake imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya kusambaza
umeme na kuwa inajikita katika kuwekeza katika vyanzo mbadala vya kuzalisha
nishati.
Awali akifungua mkutano huo, Naibu
Waziri Mkuu na Waziri wa Viwanda na Biashara wa Singapore Mhe. Gan Kim Yong
amesema kuwa mahitaji ya nishati duniani yanazidi kuongezeka siku hadi siku
hivyo nchi zinapaswa kubuni vyanzo
mbadala na kupunguza madhara yatokanayo na gesi ya ukaa ifikapo mwaka 2050.
Akitoa uzoefu wa nchi yake kwenye
kuongeza vyanzo mbadala vya nishati amesema
“ Kwa sasa tuko kwenye mkakati wa kuzalisha umeme kwa kutumia haidrojeni
na nyuklia ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kuongezeka kwa
ushiriki wa Kampuni za Google na Amazon
ambazo zimeonesha nia ya kuwekeza kwenye miradi ya nishati jadidifu.” Amesema
Mhe. Kim Yong.
Aidha, katika mkutano huo pia
umefanyika uzinduzi wa tawi la ofisi ya kanda ya Shirika la Kimataifa
la Nishati (IEA) nchini Singapore.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati
0 Maoni