WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa ametoa sababu 10 zinazoweza kumfaya mfanyabiashara yeyote
kutoka Marekani avutiwe kuwekeza nchini.
Amezitaja
sababu hizo kuwa ni mahusiano imara, sera thabiti za kiuchumi, mazingira ya
amani na uthabiti, nafasi ya kijiografia ya nchi, uwepo wa masoko makubwa,
uwepo wa nguvu kazi ya vijana na miundombinu ya kidijitali. Nyingine ni
miundombinu ya kisasa ya mawasiliano, uchumi mpana na utawala bora na mfumo wa
kodi wa haki.
Akifungua
jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Marekani lililofanyika jana
jana (Septemba 26, 2024) katika makao makuu ya ofisi za CITI, jijini New York,
Marekani, Waziri Mkuu aliwaeleza wafanyabiashara hao kwamba Tanzania ni mahali
sahihi pa kuwekeza mitaji yao na pana mvuto ambao hakuna mwekezaji anaweza
kuukwepa.
Akielezea
kuhusu uimara wa mahusiano, Waziri Mkuu alisema uhusiano wa muda mrefu baina ya
nchi hizo mbili ambao umedumu kwa zaidi ya nusu karne, unathibitisha mazingira
rafiki kwa uwekezaji.
Kuhusu sera
thabiti za kiuchumi, Waziri Mkuu alisema kwa zaidi ya miongo miwili wastani wa
ukuaji wa uchumi ulikuwa asilimia 7 na mfumuko wa bei wa chini ulikuwa wastani
wa asilimia 3.8 hadi kufikia Desemba, 2023. “IMF inakadiria kuwa kwa kiwango
hiki cha ukuaji, Tanzania itakuwa na uchumi mkubwa zaidi Afrika Mashariki
ifikapo mwaka 2028.”
Kuhusu suala
la amani, alisema mazingira ya biashara ya Tanzania ni ya kutabirika, ya uwazi
na yenye ulinzi dhidi ya kutaifisha mali, huku wawekezaji wakiruhusiwa
kurudisha faida zao baada ya kulipa kodi. “Tanzania iko kwenye eneo la
kistratejia kutokana na nafasi yake ya kijiografia. Inapakana na nchi nane,
jambo ambalo linatoa fursa bora za biashara na kuwa kitovu cha biashara cha
kikanda,” alisisitiza.
Kwenye
upatikanaji wa masoko makubwa, Waziri Mkuu alisema Tanzania inafikia soko la
ndani lenye zaidi ya watu milioni 62, na zaidi ya watu milioni 500 kupitia
jumuiya za kikanda kama vile SADC na EAC. Kuhusu nguvu kazi ya vijana, alisema
Tanzania ina idadi kubwa ya vijana, ikitoa nguvu kazi ya kutosha inayoungwa
mkono na uwekezaji katika elimu.
Akifafanua
kuhusu miundombinu ya kidijitali, alisema Serikali inafanya uwekezaji mkubwa
katika miundombinu ya kidijitali, jambo linaloifanya nchi kuvutia wawekezaji wa
teknolojia. Kuhusu miundombinu ya kisasa ya mawasiliano, Waziri Mkuu alisema
Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR), maboresho ya Shirika la Ndege la Tanzania (Air
Tanzania) na uwekezaji katika usafiri wa maji ni hatua zinazolenga kuimarisha
biashara na usafirishaji nchini.
Akiwaelezea
kupanuka kwa uchumi, Waziri Mkuu alisema Tanzania ina sekta mbalimbali zikiwemo
kilimo, madini, utalii, viwanda na utoaji wa huduma ambazo zote zinachangia
ukuaji wa uchumi. Kuhusu utawala bora na mfumo wa kodi wa haki, alisema
mabadiliko ya hivi karibuni yameboresha taratibu za kodi na kupunguza mizigo ya
kodi kwa wawekezaji, huku nchi ikijitolea kwa uwazi na haki katika utawala.
Katika hatua
nyingine, Waziri Mkuu alisema kupitia Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uzalishaji
kwa Mauzo ya Nje (EPZA), makampuni ya kimarekani yamewekeza kwenye taasisi tano
ambazo ni Tanchoice, Kibidula Farm Limited, Africado Limited, Kokoa Kamili
Limited na Next Gen Solawazi Limited ambapo uwekezaji wao kwa pamoja unafikia
dola za Marekani milioni 31.51 na umesaidia kuzalisha ajira 866.
“Makampuni
haya yanauza bidhaa nje ya nchi zenye thamani ya dola za Marekani milioni 28.6
na hasa Amerika Kaskazini, Ulaya, Masharki ya Kati na Afrika Kusini. Makampuni
haya yamewekeza kwenye usindikaji wa nyama, mazao ya parachichi na kakao pamoja
na kufua umeme wa jua.”
Akimkaribisha
Waziri Mkuu kuzungumza na wafanyabiashara hao, Waziri wa Nchi (OR-Mipango na
Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo alisema Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya kuvutia
wawekezaji na kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na washirika wa maendeleo kote
duniani ikiwemo Marekani.
“Rais Dkt.
Samia anawaona wawekezaji na viongozi kwenye sekta ya biashara siyo tu wawekezaji
muhimu lakini pia sehemu muhimu ya kuvutia wawekezaji wengine duniani.”
CHANZO:
Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni