WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa
wadau wa maendeleo washirikiane kikamilifu na nchi zinazoendelea katika
kusaidia utekelezaji wa mifumo jumuishi ya kifedha.
Ametoa wito huo Septemba 25, 2024, wakati
akifungua mjadala kuhusu miaka 15
ya mafanikio katika masuala ya Mfumo
Jumuishi wa Fedha kwa Maendeleo kwenye mkutano ulioitishwa na Malkia wa
Uholanzi, Mhe. Maxima ambaye ni mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
katika Huduma Jumuishi za Fedha, Jijini New York, Marekani
Amesema kuwa
uchumi jumuishi ni muhimu hasa katika utekelezaji wa mpango endelevu wa
maendeleo na ufanikishaji wa ajenda 2030.
“Huduma jumuishi za kifedha ni kiungo muhimu cha ukuaji wa uchumi,
kupunguza umasikini na kuleta maendeleo ya jamii kwa ujumla.”
Aidha,
Mheshimiwa Majaliwa amempongeza Malkia Maxima kwa juhudi zake ambazo
zimewezesha ongezeko kubwa la ufikiaji wa huduma za kifedha duniani, huku zaidi
ya asilimia 50 ya watu wakiwa wamefikiwa na mpango huo katika kipindi cha
muongo mmoja uliopita.
“Umiliki wa
akaunti duniani umeongezeka kutoka asilimia 51 mwaka 2011 hadi kufikia asilimia
76 kwa mwaka 2021. Haya ni mafanikio makubwa, changamoto imebaki hasa kwa
wanawake waishio katika nchi zinazoendelea ambapo wengi wao bado hawajaingizwa
kwenye mfumo jumuishi wa kifedha.”
Mapema,
Malkia Maxima wa Uholanzi alisema anafurahishwa na hatua iliyofikiwa sasa
ikilinganishwa na hali ilivyokuwa hapo awali.
"Wakati
tunaanza hii kazi ya kuhimiza mifumo jumuishi ya kifedha hatukuwa na takwimu
zozote. Tulipanda na kufikia asilimia 50 na sasa tunakaribia asilimia 80.
Natambua asilimia 80 siyo sawa na asilimia 100, ni lazima nikiri kuwa kazi
imefanyika," alisema.
Akionesha
dhahiri kuwa bado kazi haijaisha, Malkia Maxima alisema mkakati uliopo ni
kuwafikia watu bilioni 1.5 ambao bado hawajafikiwa na huduma jumuishi za
kifedha.
Alisema
anafarijika kuona watunwa rika mbalimbali wakitumia mifumo hii kwenye maeneo
ambayo huduma za kifedha zinapatikana. "Mabibi wanaweka fedha na kusomesha
wajukuu zao, vijana na mabinti wajasiriamali wanatumia huduma hizo kutunza
fedha zao, kupata mikopo midogo midogo na kukuza mitaji yao," alisema.
0 Maoni