Mwenyekiti
wa CCM Mkoa wa Mbeya, Bw Patrick Mwalunenge amefungua Tamasha la Utamaduni wa
Mtanzania kwa jamii ya Wanyakyusa Kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam na
kuwaasa Watanzania kutunza mazingira kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.
Akifungua
tamasha hilo jana Bw. Mwalunenge amesema kuwa utunzaji wa mazingira ni wajibu
wa kila Mtanzania na kwamba matumizi ya malighafi ya asili yanayopatikana
katika maeneo yao yatasaidia kutunza mazingira na kuendeleza utamaduni wa
Mtanzania.
"Watanzania
ni lazima turudi kwenye matumizi ya vifaa vya asili ili tuweze kutunza
mazingira yetu" Amesisitiza Bw. Mwalunenge.
Naye Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Bi. Frida Kombe amesema
malengo ya Tamasha hilo ni kutoa nafasi kwa jamii za Tanzania kuonesha tamaduni
zao katika Kijiji cha Makumbusho.
Alisema
kwamba “Tamasha la Siku ya Utamaduni wa Mtanzania ni mojawapo ya utekelezaji
kwa vitendo wa sheria yetu ya Makumbusho ya Taifa la Tanzania na Malikale
lakini pia ilani ya CCM inayoweka bayana ushirikishwaji wa jamii kwenye
uhifadhi wa urithi wa Utamaduni na kuutumia urithi huo kama chanzo cha
mapato,"
Bi Kombe
ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mhe. Dr. Samia
Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiongezea Taasisi ya Makumbusho uwezo wa
kutekeleza majukumu ya uhifadhi wa urithi wa asili na utamaduni.
Tamasha la
Utamaduni wa Mtanzania kwa jamii ya Wanyakyusa litafanyika kwa muda wa siku
tatu kuanzia tarehe 27 hadi 29 Septemba 2024 ambapo wananchi wanaweza kujifunza
mila na desturi, vyakula, ngoma na mavazi ya jamii wa Wanyakyusa.Watu wote
wanakaribishwa hamna kiingilio.
0 Maoni