Zoezi la
kuelimisha wananchi kuhama kwa hiari ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro limeendelea
kueleweka ambapo leo tarehe 28 Septemba 2024 kaya 28 zenye watu 130 na mifugo
346 zimehama kwa hiari kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera
Wilaya ua Handeni na Makao Wilaya ya
Meatu.
Kwa mujibu
wa kamishna msaidizi mwandamizi wa uhifadhi (Idara ya Maendeleo ya jamii)
Gloria Bideberi kati ya kaya 28 zilizohama leo, kaya 26 zenye watu 119 na
mifugo 329 zimehamia kijiji cha Msomera Handeni na Kaya 2 zenye watu 11 na
mifugo 17 zimehamia kijiji cha Makao Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu.
Ameongeza
kuwa tangu zoezi hilo lilipoanza mwezi Juni 2022 hadi kufikia tarehe 28
Septemba, 2024 Jumla ya kaya 1,655 zenye watu 9,976 na mifugo 40,397
zimeshahama kwa hiari ndani ya hifadhi ya Ngorongoro.
Kamishna
Bideberi amefafanua kuwa kwa sasa wananchi wanaojiandikisha kuhama kwa hiari
zoezi ni la muda mfupi ambapo kila kaya zinazojiandikisha zinahamishwa katika
muda wa wiki mbili.
“Serikali imeendelea kuwezesha zoezi hili ndio
maana mnaona hata tukipata kaya chache zinazojiandikisha hatuna haja ya
kuwasubirisha mda mrefu, tunawahamisha kwa haraka wakati wengine wakiendelea
kujiandikisha kwa kuwa zoezi hili ni endelevu na linafanyika kwa umakini
mkubwa” ameongeza Bideberi.
Akiaga kundi
hilo kwa niaba ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Mkurugenzi wa Idara ya
Wanyamapori Dkt. Alex Lobora amewapongeza wananchi wote wa Ngorongoro kwa
kuendelea kuhama kwa hiari kwa ajili ya kupisha na kuimarisha shughuli za
uhifadhi lakini pia kuboresha Maisha yao katika
maeneo bora zaidi na salama nje
ya Hifadhi.
Dkt. Lobora
amebainisha kuwa uamuzi wa wananchi hao kuhama unaashiria matokeo chanya
ya kuiokoa hifadhi ya Ngorongoro kwa
maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo kwa kuwa
Ngorongoro ni eneo la urithi wa dunia ambalo kutokana na uhifadhi
endelevu limeendelea kuvutia watalii wengi na Serikali kupata mapato
yanayoiwezesha kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi wa Ngorongoro na
Watanzania kwa ujumla.
‘Nawasihi
muendelee kuwa mabalozi katika kushawishi ndugu zenu waliobaki ili nao wahame
kwa ajili ya kuimarisha shughuli za uhifadhi wa Wanyamapori, mazingira, misitu,
malikale na ikolojia ya Ngorongoro ambayo tunaamini uhai endelevu wa Ngorongoro
unazinusuru pia hifadhi za maeneo ya jirani inazopakana nazo” aliongeza Dkt.
Lobora.
Kwa upande
wake mwakilishi wa Kamishna wa Uhifadhi NCAA, Kamishna Msaidizi Mwandamizi
Lilian Magoma amesema hatua ya Wananchi kuhama ndani ya hifadhi imezingatia
ushirikishwaji kwa kuwaelimisha umuhimu wa kupisha shughuli za hifadhi katika
eneo la Ngorongoro ili wananchi waweze kujiendeleza katika Maisha bora zaidi na
salama nje ya hifadhi.
“Wananchi
walio wengi wanatambua kuwa sheria za uhifadhi zinakataza baadhi ya shughuli za
kiuchumi kufanyika kama ujenzi wa nyumba za kudumu, Kulima, kuingiza umeme,
kumiliki vyombo vya moto, na kuamua kuhama kwenda maeneo mengine, Serikali
tutaendelea kuimarisha uhusiano na wananchi wa Ngorongoro na kuhakikisha
tunawashirikisha katika kila hatua ya utekelezaji wa mpango wa kuhama kwa hiari
kwa ajili ya kupisha shughuli za uhifadhi na kuimarisha ustawi wa Maisha yenu”
amefafanua Magoma.
Magoma
amehitimisha kwa kueleza kuwa wananchi wanaohama ndani ya Hifadhi wametengewa
eneo la kutosha kwa ajili ya malisho ambao Kijiji cha Msomera kuna hekta 22,000, Kijiji cha Saunyi hekta 9,000 na
Kijiji cha kitwai hekta 53,000 za malisho hali inayotosheleza malisho kwa mifugo ya Wananchi wanaoendelea
kuhamia maeneo hayo.
Na.
Mwandishi Wetu- NCAA
0 Maoni