Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewahimiza viongozi wa Dini
nchini kuendelea kusimamia misingi ya malezi na makuzi ya kwa watoto ili
kuhakikisha tunu ya amani iliyopo nchini inalindwa na kuhifadhiwa.
Dkt. Biteko
amesema hayo wakati akizungumza katika ufungaji wa Kanisa la Pentecostal
Assemblies of God (Tanzania) uliofanyika Jijini Dodoma, ambapo amesema Kanisa
linatakiwa kulinda amani iliyopo na daima viongozi wa dini wasikubali tofauti
za kibinadamu zitumike kuondosha amani ya nchi.
“Kuna watu
ni wakandarasi wa uongo na wengine ni mawakala wa uongo; PAG tukawafundishe
watu kuwa uongo wa aina hiyo, unaweza kusababisha uvunjifu wa amani na kuna
watu wangependa tofauti zetu za dini, kabila na mitazamo yetu igeuzwe mtaji wa
kisiasa, tusikubali na tuendelee kuwa wamoja na kuilinda tunu ya amani yetu”
amesema Dkt. Biteko.
Amesema
Tanzania ni kama familia inayojengwa na kila mtu wakiwemo viongozi wa Dini na
Taifa bora litapatikana kutokana na familia bora huku akikisisitiza umuhimu wa
kuzilinda mila nzuri na kujiepusha na tamaduni zinazosababisha mmomonyoko wa
maadili ya jamii.
“Baadhi ya
nchi Duniani zimekumbwa na machafuko lakini sisi tuna bahati kuishi kwa amani
hatudhuriani kutokana na tofauti zetu na amani tuliyonayo ni tunu, hivyo Kanisa
lione umuhimu wa kulinda tunu hii na anayetaka kuvunja amani hiyo tofautianeni
naye,” amesema na kuongeza kuwa viongozi wa dini wakawambie waumini kwamba
jambo la msingi katika familia na taifa ni maendeleo na amani na hivyo wahimize
wananchi kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika
baadaye mwaka huu ukifuatiwa na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwakani.
Akizungumza wakati wa akimkaribisha mgeni rasmi, Askofu Mkuu wa PAG(Tanzania) Dkt. Daniel Awet ameiomba Serikali kuendeleza mazingira rafiki kwa Watanzania ili kuimarisha Demokrasia, haki na misingi ya amani iliyodumu kwa miaka mingi.
Aidha,
amemwomba Dkt. Biteko afikishe salamu za Kanisa hilo kwa Rais, Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan akimweleza kuwa waumini wanatambua kazi kubwa na nzuri
inayofanywa na Serikali anayoingoza na wao kama raia wake wanashirikiana naye
kujenga na kulinda amani ya nchi.
Askofu Dkt.
Awet pia amewasilisha changamoto ya mgogoro wa kiwanja katika eneo la sabasaba
Jijini Dodoma na uvamizi wa kiwanja kingine kinachodaiwa kuvamiwa na wachimbaji
wa madini ambapo Dkt. Biteko ameelekeza ufuatiliaji wa changamoto hiyo na yeye
apatiwe nakala za Barua husika kwa ajili ya hatua za maamuzi.
0 Maoni