Baraza la
Madiwani kutoka Wilaya ya Kaskazini A' Unguja wametembelea TFS- Shamba la Miti
Sao hill leo tarehe 25 Septemba 2024 kwa lengo la kujifunza namna ambavyo
shughuli za utunzaji na uhifadhi wa mazingira zinavyofanywa na Wakala wa Huduma
za Misitu Tanzania.
Akizungumza
katika ziara hiyo Mstahiki Meya wa Manispaa ya Wilaya ya Kaskazini A' Unguja
Bw. Machano Fadhili Machano (BABLA) amesema kuwa lengo kuu la ziara hiyo ni
kujifunza namna ya ukusanyaji wa mapato, kwani asilimia kubwa ya mapato katika
Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi inatokana na mazao ya misitu ikichagizwa na uwepo
wa Shamba la serikali la miti ya kupandwa la Sao hill.
Aidha
ameongeza ziara hiyo wanatarajia kujifunza juu ya suala zima la utunzaji wa
mazingira kupitia shughuli za uhifadhi kwani TFS kupitia Shamba la miti Saohill
limekuwa na utaratibu wa kushirikisha wananchi katika jukumu la uhifadhi wa
misitu na hivyo itawasaidia kufanya
ushirikishaji kwa wananchi ili kuhakikisha misitu na mazingira inatunzwa.
Naye
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Mhe. Festo Elia Mgina amesema
kuwa ziara hiyo ni matokeo ya uhusiano mzuri baina ya Halmashauri ya Wilaya ya
Mufindi na Wilaya ya Kaskazini A' Unguja hivyo imelenga katika kujifunza namna
Wilaya ya Mufindi imekuwa ikifanikiwa katika ukusanyaji wa mapato ya
Halmashauri kupitia mazao ya misitu.
"Tumewaleta
wageni wetu wajifunze katika Shamba la TFS- Sao hill ili waone ni jinsi gani
limekuwa likichangia mapato makubwa katika Halmashauri zetu lakini pia jinsi
linavyochangia katika huduma mbalimbali za jamii katika wilaya yetu ikiwemo
ujenzi wa mabweni, madawati, zahanati, miondombinu ya barabara na elimu ya
uhifadhi wa mazingira kwa kupanda miti," amesema M/kiti Mgina.
Akizungumza
kwa niaba ya Mkurugenzi wa Kaskazini A' na Madiwani wote Afisa Utawala wa
Baraza la Manispaa ya Kaskazini A' Husna Khamis Mohammed, amesema kuwa ziara hiyo ina tija kubwa sana
kwa madiwani wote kwani itawasaidia kubuni vyanzo vipya vya mapato na namna
bora ya utunzaji wa mazingira ili kusaidia maendeleo ya wananchi wao kama
ilivyo Mufindi.
Kwa upande
wake Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Saohill PCO. Tebby Yoramu wakati
akiwakaribisha wagaeni hao ameongeza kuwa ni faraja kubwa kwa shamba na TFS kwa
ujumla, kwani unasaidia katika kuimarisha ushirikiano katika shughuli za
uhifadhi pamoja na kuongeza mnyororo wa thamani unaotokana na uzalishaji wa
mazao ya misitu kwani Zanzibar ni miongoni mwa wanufaika wakubwa wa mazao ya
misitu yatokayo Wilayani Mufundi hususani mbao kutoka Shamba la miti Sao hill.
Katika Ziara
hiyo Madiwani hao waliweza kutembelea na kuona jinsi shughuli za uvunaji wa
utomvu katika miti ya misindano zinavyofanywa na kuongeza pato, pamoja na
kiwanda cha kuzalisha malighafi ya nguzo za umeme cha Mufindi Woods and Poles
Co. Ltd wakiwa wameambatana na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya
Kaskazini A' Unguja Ndg. Ali Khamis Makame pamoja na Mwenyekiti wa CCM Wilaya
ya Mufindi Ndg. George Kavenuke na Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya
Mufindi.
0 Maoni