Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameagiza mikoa na
hamlashauri zote nchini kuhakikisha viwanda vilivyo katika mamlaka zao
vinashiriki katika maonesho ya biashara ya kimataifa.
Dkt. Biteko
amesema hayo leo Septemba 26, 2024 Jijini Dar es salaam wakati akimwakilisha
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory
Mpango katika ufunguzi wa Maonesho ya Pili ya Kimataifa ya Viwanda Tanzania
mwaka 2024.
“Naagiza
Mikoa na Halmashauri zote nchini kuhakikisha Viwanda vilivyo katika Mamlaka zao
vinashiriki kuonesha bidhaa wanazozalisha ili bidhaa hizo ziweze kutafutiwa
masoko ya ndani na nje ya nchi yakiwemo ya ukanda wa EAC na SADC kwa lengo la
kuongeza mauzo ya bidhaa na huduma za Tanzania nje ya nchi,” amesema Dkt.
Biteko.
Dkt. Biteko
ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita
itaendelea kuweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji hususani
katika sekta ya viwanda ili kukuza uchumi wa Viwanda na nchi kwa ujumla.
“Tutakumbuka
kuwa andiko letu la Blueprint ambalo
limeainisha changamoto mbalimbali zinazokwaza maendeleo ya sekta ya viwanda na
biashara nchini na mapendekezo ya nini kifanyike ili kuondoa changamoto hizo.
Kazi hiyo ilianza katika Awamu ya Tano na nipende kuwahakikishia kuwa Serikali
ya Awamu ya Sita inaendelea kuhakikisha kuwa changamoto zinazoikabili biashara
na uwekezaji ikiwemo katika sekta ya viwanda zinaendelea kutatuliwa,” amebainisha
Dkt. Biteko.
Aidha,
amewahamasisha wafanyabishara na wenye viwanda nchini, kuendelea kushirikiana
na Serikali na Taaasisi zake, katika kuhakikisha kuwa changamoto zinazoikabili
sekta ya viwanda nchini tunazitatua kwa pamoja ili kukuza uchumi wa nchi.
Pia, Dkt.
Biteko amebainisha kuwa maonesho hayo yatakuwa na tija zaidi ikiwa wahusika
wataaelezana ukweli ili kuwa namna bora ya kutatua changamoto mbalimbali
zinazoikabili sekta ya viwanda na biashara nchini. Sambamba na kuzitaka taasisi
zote zinazosimamia ubora wa bidhaa kuhakikisha zinashiriki katika maonesho hayo
ili kutoa elimu kwa umma na kutatua changamoto zinazoikabili katika sekta hiyo.
“Nitumie
fursa hii kuzielekeza taasisi zote za Serikali za udhibiti na wezeshi katika
sekta ya biashara, viwanda na uwekezaji kama BRELA, TBS, TMDA, TIC, WMA, FCC,
OSHA, SIDO nakadhalika, kuhakikisha zinashiriki katika Maonesho haya ili
kuendelea kutoa elimu kwa umma na kutumia fursa hiyo kutatua changamoto
zinazokabili sekta ya viwanda na wafanyabiashara kwa ujumla nchini,” amesema
Dkt. Biteko.
Akizungumzia
bidhaa zinazoingizwa kwa magendo nchini kupitia Mkoa wa Dar es salam, Dkt.
Biteko ameitaka Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es salaam kudhibiti
njia za magendo huku akiwataka wafanyabiashara kuona fahari kulipia kodi bidhaa
zinazoingizwa nchini.
Katika hatua
nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa awali Tanzania ilikuwa na uhaba wa umeme na
kuwa kwa sasa nchi inajitosheleza katika nishati ya umeme.
“Sasa tuna
ziada ya umeme ya kutosha hata mkienda kuangalia leo matumizi ya umeme
tunaozalisha kwa kutumia gesi yamepungua
kwa sababu tuna umeme wa kuzalisha wa maji wa kutosha kwa hiyo hatuna tatizo la
umeme kwa kuwa Serikali imeweka mifumo mizuri, tumieni umeme huu kwa ajili ya
kusalisha bidhaa,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Fauka ya
hayo, Dkt. Biteko ametoa wito kwa wenye viwanda nchini kutumia fursa ya
Maonesho hayo kushiriki kwa wingi ili kujifunza teknolojia mpya za kisasa,
kutangaza bidhaa zao na kuufahamisha umma na walaji juu ya ubora na faida za
kutumia bidhaa zinazozalishwa na viwanda mchini. Aidha, Serikali inatambua
kwamba sekta binafsi ndiyo muhimili mkubwa wa kujenga uchumi wa viwanda huku
yenyewe ikiwekeza katika kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara.
Pia, Dkt.
Biteko amewahamasisha wadau wa sekta ya viwanda kuendelea kutoa michango yao ya
mawazo ya namna ya kuboresha Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo. Pamoja na
kuwataka Watanzania kujitokeza kupiga kura na kuchagua viongozi wazalendo
katika ngazi za mitaa na vijiji.
Naibu Waziri
wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud
Kigahe amesema kuwa maonesho hayo yamehusisha washiriki 250 kutoka
kampuni za ndani na nje ya nchi na kutaja lengo la maonesho hayo kuwa ni
kujifunza na kubadilishana mawazo katika sekta ya viwanda.
“Tunategemea
mwakani kuona hamasa zaidi kwa wazalishaji wadogo ambao ni zaidi ya asilimia
90, naomba niwahakikishie Wizara ya Viwanda itaendelea kushirikiana na wadau
mbalimbali wanaounga mkono sekta ya viwanda nchini,” amesema Mhe. Kigahe.
Mkuu wa Mkoa
wa Dar es salaam, Mhe. Albert Chalamila amesema kuwa maonesho hayo yahimize
uzalishaji wa bidhaa za ndani ya nchi zenye ubora ili zishindane na masoko ya
nje.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Tantrade, Prof. Ulingeta Mbamba amesema kuwa maonesho hayo ya
pili yameandaliwa kwa ushirikiano kati ya
Tanrtrade na kuwa ni muhimu kwa vile
yanahamasisha wazalishaji wa bidhaa za viwanda na wazalishaji binafsi kwa ajili ya kupata masoko ya ndani
na nje ya nchi.
Mwenyekti wa
Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI),
Bw. Paul Makanza amesema kuwa kuna fursa ya kutengeneza bidhaa na kuuza
nje ya nchi na kuwa maonesho hayo ni jukwaa muhimu la kujenga
mtandao wa wateja na wafanya biashara na kujifunza kutoka kwa wageni.
Awali Dkt.
Biteko ametembelea mabanda mbalimbali na kuona magari yanayotumia umeme yanayozalishwa
nchini na Kampuni ya KAYPEE Motors Limited
pamoja na ndege zinazotengenezwa mkoani Morogoro na kmpuni kutoka nchini
Czech.
Maonesho haya ya Pili (2) ya Kimataifa ya Viwanda Tanzania 2024 yanatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 01, 2024.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akiwa ndani ya ndege ndogo iliyotengenezwa Tanzania, katika ufunguzi wa Maonesho ya Pili ya Kimataifa ya Viwanda Tanzania mwaka 2024.
0 Maoni