Tanzania imepokea pongezi kutoka kwa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kuboresha uhifadhi wa misitu asilia kupitia Mradi wa Kuimarisha Ustahimilivu wa Bioanuai ya Misitu ya Mazingira Asilia Tanzania Dhidi ya Athari za Mabadiliko ya Tabianchi.
Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Shigeki Komatsubara anasema kuwa
ziara yao kwenye misitu ya asilia wa mlima wa Hanang' uliokuwa umeathirika na
mafuriko yaliotokea Wilaya ya Hanang' mapema mwaka huu, ilithibitisha
mabadiliko makubwa na urejeshwaji wa uoto wa asili, ikionyesha jitihada za
dhati zinazofanywa na Tanzania katika uhifadhi wa mazingira.
“Katika siku hizi tatu, tumeridhishwa sana na urejeshwaji wa
bionuwai katika mlima huu wa Hanang na ujumuishi wa uoto wa asili. Tunaamini
tutaendelea kushirikiana katika kuongeza na kukuza fursa za uchumi,"
anasema.
Serikali ya Tanzania, kupitia Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala
wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo, imeeleza kuwa
itatumia uzoefu uliopatikana kupitia mradi huu kuboresha zaidi uhifadhi wa
misitu ya asili, kuongeza thamani ya misitu, na kukuza fursa za uchumi kupitia
utalii wa misitu.
Prof. Silayo alisisitiza kuwa, “Misitu hii asilia imekuwa
kivutio kikubwa. Kwa mfano, katika msitu wa mlima wa Hanang', wageni
wameongezeka, miundombinu imeboreshwa, hewa ni safi, na ulinzi umeimarishwa.
Tutahakikisha maeneo haya tunayafungua zaidi kwa ajili ya matumizi bora.”
Aidha, Prof. Silayo aliongeza kuwa, kupitia ushirikiano kati
ya TFS na UNDP, Serikali itaweka utaratibu endelevu wa usimamizi wa misitu na
kuongeza thamani ya misitu hiyo ya asili huku ikishirikisha wananchi katika
juhudi za kuitunza.
Tanzania ina misitu asilia 24, ambapo misitu 19 imeendelezwa
kwa ushirikiano wa TFS na UNDP kupitia mradi wa kuimarisha bianowai ya misitu
ya mazingira asilia dhidi ya tishio la mabadiliko ya tabia nchi.
0 Maoni