Katika kuadhimisha
miaka 60 ya kuanzishwa kwa Jeshi la Polisi nchini, Kituo cha Polisi Mikumi kwa
kushirikiana na maafisa na askari wa Uhifadhi, Hifadhi ya Taifa Mikumi
wamefanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kufanya usafi katika kituo cha
Afya Mikumi mkoani Morogoro kwa lengo kuyaweka mazingira yawe safi na salama
ili kulinda afya ya wagonjwa, wafanyakazi na watumiaji wengine wa eneo hilo.
Zoezi hilo la usafi limefanyika leo Septemba 14, 2024
likiongozwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi Rehembe SSP Kashorael Mnuo
akiwa katika zoezi hilo alisema, “Tumeamua kuungana na Majeshi USU mengine
wakiwemo hawa wenzetu maafisa na askari
wa Hifadhi ya Taifa Mikumi ili kuweka mazingira safi na salama kuepuka magonjwa
ya milipuko yanayosababishwa na uchafu.”
SSP Mnuo aliongeza kuwa Jeshi la Polisi nchini wamekuwa na
desturi ya kushirikiana na vyombo vingine
vya ulinzi na usalama kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo
kufanya usafi katika maeneo haya na mengine mengi kwa lengo la kuwa karibu na
jamii katika wiki hii ya kuadhimisha miaka 60 ya kuanzishwa kwa jeshi hilo.
“Tupo kwenye wiki ya maadhimisho ya miaka 60 ya kuanzishwa
kwa jeshi letu hapa nchini, tumeamua kushirikiana na wenzetu wa Hifadhi ya
Taifa Mikumi kufanya usafi eneo hili la Kituo cha afya ikiwa ni pamoja na
kuwapa pole wagonjwa kwani kufanya hivi
ni kuonyesha upendo wetu kwa jamii na pia ni matendo ya huruma ambayo
vitabu vyote vya kiimani vinatutaka tufanye,” alisisitiza Kamanda Mnuo.
Aidha, alisema kuwa kilele cha maadhimisho hayo itakuwa ni
Septemba 17 mwaka huu na kwamba mbali na
kufanya usafi huo pia watawatembelea watu wenye mahitaji maalumu na kuweza
kuwasaidia ambapo aliishukuru Mikumi kwa kuungana nao katika zoezi hilo la
usafi.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Hifadhi ya Taifa
Mikumi, Augustine Massesa alisema kuwa wao kama wahifadhi wanalishukuru jeshi
la polisi kwa kuwashirikisha katika zoezi hilo la kijamii ambapo alieleza kuwa
Mikumi imekuwa mstari wa mbale katika kushiriki shughuli za kijamii.
Kamishna Massesa alisema kuwa kitendo cha wao kushiriki
katika shughuli za kijamii maeneo yanayowazunguka yameendelea kuwa chachu ya
kuitangaza Hifadhi ya Taifa Mikumi na kudumisha mahusiano ya kuwafichua baadhi
ya wananchi wachache wanaojihusisha na shughuli haramu za ujangili katika
Hifadhi hiyo.
“Sisi kama Mikumi tutaendelea kushiriki shughuli mbalimbali
za kijamii kwani kufanya hivi mbali na kuitangaza Hifadhi ya Taifa Mikumi pia
ni moja ya njia ya kudumisha mahusiano baina yetu na jamii inayotuzunguka na
hivyo kudhibiti ujangili.”
Kwa upande wake Mganga wa kituo hicho cha afya Mikumi Beno Hamfik, kwa niaba ya Mganga Mfawidhi alilishukuru jeshi la polisi pamoja na Hifadhi ya Taifa Mikumi kwa kuendesha zoezi la usafi ambapo aliomba zoezi hilo la usafi liwe endelevu kila mara hata kwa wadau wengine.
Na. Zainab Ally - Mikumi
0 Maoni