Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Dodoma imetoa elimu ya vipimo
kwa Watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), hivyo
kutimiza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan yanayozitaka Mamlaka na Taasisi
za Umma kupanga na kutekeleza kwa pamoja majukumu mbalimbali ya Serikali.
Akifungua Semina hiyo ya siku moja iliyofanyika jijini
Dodoma, Katibu Tawala wa Mkoa, Kaspar Mmuya amepongeza ushirikiano wa Taasisi
hizo mbili unaolenga kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais na kuwahudumia
wananchi ipasavyo.
“Nimefurahishwa na ushirikiano wa Taasisi hizi mbili wenye
lengo la kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais kuhusu dhana ya kufikiri kwa
pamoja na kutenda kwa pamoja kama Serikali.”
Aidha, Katibu Tawala Mmuya amewataka washiriki kutumia
semina hiyo kupambanua endapo kuna mapungufu yoyote katika Sheria ya Vipimo
inayosimamiwa na WMA na kutafuta suluhisho la pamoja ili kuboresha utekelezaji
wake.
Vilevile, amewataka WMA kuendelea kutoa elimu ya vipimo kwa
wafanyabiashara na walaji ili pande zote mbili zipate kilicho stahiki. Pia,
ameongeza kwamba katika utoaji elimu, wakulima waeleweshwe kuachana na
utamaduni wa kutumia madalali bali wauze mazao yao katika maghala.
“Mheshimiwa Rais ametoa maelekezo kwamba mazao yauzwe kwenye
maghala na huko kwenye maghala kuwe na mizani ambazo zimekaguliwa na kuhakikiwa
na Wakala wa Vipimo ili kumlinda mlaji na mfanyabiashara,” ameeleza Mmuya.
Mmuya ametoa wito kwa wafanyabiashara, walaji wa bidhaa na
huduma mbalimbali kuzingatia matumizi ya vipimo sahihi na kuwakumbusha kwamba
sheria ya vipimo imewapa WMA mamlaka ya kutoza faini kwa yeyote atakayekiuka
mwongozo wa sheria hiyo.
Amewataka WMA na TAKUKURU kuwa mfano kwa sheria
wanazozisimamia na kuchukuliana hatua baina yao endapo kutabainika ukiukwaji wa
sheria.
“TAKUKURU, mtumishi yeyote wa WMA akitenda ndivyo sivyo kwa
kujihusisha na rushwa basi achukuliwe hatua, vivyo hivyo kwa WMA, mkibaini
mtumishi wa TAKUKURU anajihusisha na uvunjifu wa sheria ya vipimo katika
shughuli zake kama mtanzania wa kawaida ikiwemo kilimo, biashara na nyinginezo,
msisite kumchukulia hatua,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Meneja wa WMA Mkoa wa Dodoma, Karim Zuberi
amesema lengo la kutoa semina hiyo kwa watumishi wa TAKUKURU ambao ni watumiaji
wa vipimo, ni kuwapatia uelewa ili wajue haki zao wanaponunua bidhaa au kupata
huduma mbalimbali.
“Kupitia semina hii watapata uelewa ni kwa namna gani kipimo
kinatakiwa kuwa kabla, wakati na baada ya kununua bidhaa au kupata huduma,”
amesema Zuberi.
Vilevile, amesema malengo mengine ni kutekeleza moja ya
majukumu ya WMA ambalo ni utoaji elimu ya vipimo kwa jamii kupitia makundi
mbalimbali kama wafanyabiashara, viongozi, wanasiasa, watumishi wa umma na
mengineyo ambapo TAKUKURU ni kundi mojawapo.
Amesema, lengo jingine ni kupata maoni ya TAKUKURU kuhusu
namna bora ya kutekeleza sheria ya vipimo endapo watabaini mapungufu wakati wa
uwasilishwaji mada katika semina husika.
Naye Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma, Victor Swela
ameishukuru WMA kuona umuhimu wa kuandaa semina hiyo ili kuwajengea uelewa wa
masuala ya kivipimo hivyo kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kiufanisi katika
sekta hiyo.
“Tutashirikiana na wenzetu wa WMA kuwaelimisha wananchi na kusimamia kuhakikisha kila upande unazingatia matumizi ya vipimo sahihi kwa manufaa ya pande zote yaani wafanyabiashara na walaji.”
Na. Veronica Simba- WMA Dodoma
0 Maoni