Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi Tanzania Jumuiya ya CCM, Ndugu. Ally Salum Hapi (MNEC) ametuma salamu kwa viongozi wasio wajibika katika nafasi zao walizoaminiwa na wananchi huku akisema Chama cha Mapinduzi hakitambeba mtu katika uchaguzi unaokuja.
Hapi ametuma salamu hizo akiwa katika mkutano na viongozi na
wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bagamoyo uliofanyika katika ukumbi
wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TASUBA) Mkoani Pwani,
"Chama chetu kina utaratibu mzuri sana katika chaguzi
muda unapofika na kila muda wa uchaguzi ndiyo maana tunasisitiza suala la
kupata wagombea bora tutakao wauza kwa urahisi ambaye anakubalika na wananchi
na siyo anayekubalika kwenye mifuko ya watu wachache, kiongozi ambaye anazijua
shida za wananchi na uchaguzi wa serikali za mitaa ndiyo msingi wa uchaguzi
mkuu," alisema Hapi.
Kuhusu viongozi wasiowajibika kwenye nafasi zao Hapi
alitumia mkutano huo kukumbusha kuwa katika kipindi kilichosalia kuelekea
uchaguzi Mkuu mwaka ujao ni muhimu kwa kila kiongozi aliyechaguliwa na wananchi
kujitathimini iwapo anafaa kurejea katika nafasi yake kwenye uchaguzi ujao,
iwapo wananchi watamuunga mkono kutokana na kazi zake.
"Waheshimiwa madiwani naomba mchape kazi muda ndiyo huu
chama hakitambeba mtu ambaye hakujibeba yeye mwenyewe kwa utendaji kazi wake,
wala hakitambeba mtu anayejisemea mwenyewe ambae hakisemei chama, hamsemei
Mbunge wala hamsemei Rais wa CCM ninachoomba mtambue ni kuwa unafika kwenye
uchaguzi huchaguliwi wewe kwa sababu ni bingwa wa fitna au wewe ni bingwa wa
kumsema vibaya mwenzio au wewe ni bingwa wa kujisemea wewe mwenyewe tu bali
matendo yako na namna ulivyoshughulika na matatizo ya wananchi pamoja na kazi
unazozifanya kwa hiyo tupeleke wagombea wanaokubalika wenye sifa na wanaojua
uongozi na wanajua kuishi na watu, kila mwenye sifa nendeni mkawahamasishe
wagombee," alisema Hapi.
Katika hatua nyingine Hapi aliwanyooshea kidole na kuwaonya
watu wanaojihusisha na udalali kwenye uchaguzi kwa kujifanya wao ndiyo kila
kitu juu ya ushindi wa wagombea kwa kuwa wanajua namna ya kuzungumza na
wananchi hali hiyo imekuwa mzigo mkubwa kwa viongozi walioko madarakani na
kusababisha washindwe kufanya kazi kwa ufasaha.
"Lakini wapo watu hapa ni madalali wa uchaguzi ambao wametengeneza upepo kwa mtu yeyote anayetaka kugombea nafasi hiyo lazima amuone yeye na akiamini ushindi wa mgombea upo kwenye mikono yake, katika kipindi hiki jiepusheni na madalali wa siasa katika uchaguzi," alisema Hapi.
0 Maoni