Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko ameiasa jamii kuwa na utaratibu wa kuwatunza na kuwajali wazazi wao na
kuendelea kuwaombea ambao hawapo hai.
“Tuendelee kuwakumbuka na kuwaombea ndugu na wazazi
waliotangulia mbele za haki ni jambo zuri na wajibu wetu tuliobaki, Sheikh wetu
katika mawaidha yake ameliongelea kwa uzuri sana. Tulitilie maanani na sote
tuendelelee kufanya hivi, na kama huwa hatuwafanyii hivi ndugu zetu, hatuna
budi tuanze kwa moyo wote,” amesema Dkt. Biteko.
Dkt. Biteko ameyasema hayo jana Septenba 7, 2024 akiwa
Nyakatuntu, Kyerwa mkoani Kagera wakati aliposhiriki katika dua ya kuwaombea
baba mzazi na ndugu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Bw. Abdulmajid
Mussa Nsekela.
Ameongeza “Ndugu zangu tusisahau mapito yetu. Katika mapito
huwa kuna watu. Katika watu hawa, kuna wazazi wetu. Kama wazazi wako wapo hai,
mmoja au wote au wale waliokulea, jua nawe una wajibu wa kuwalea na kuwatunza,
siyo kifedha tu bali pia kwa mahusiano mema hasa ya kihisia kwa kuwa hivyo
ndivyo impendezavyo Mungu.”
Ametolea mfano “Mzee wetu, Rais wa Awamu ya Pili, Marehemu
Ally Hassan Mwinyi, Mzee Rukhsa alituasa kuwa maisha yetu hapa duniani si kitu
ila ni hadithi tu na kuwa tuyafanye maisha yetu yawe hadithi nzuri. Kwa dua
hii, kwa umati huu, kwa wanafamilia hawa wa Nsekela inadhihirisha bayana kabisa
kuwa maisha ya Mzee wetu, Alhaji Tibihika Mussa Nsekela, na wengine
tuliowaombea dua leo hapa yameacha hadithi nzuri kwa sisi tuliobaki hili ni
jambo zuri la kujifunza.”
Aidha, Dkt. Biteko ameendelea kuiasa jamii Kushiriki katika
shughuli za maendeleo katika maeneo yao wanapotoka, kuendelea kuishi kwa upendo
sambamba na kuishukuru familia hiyo kwa kumualika kushiriki katika dua hiyo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali imeendelea na jitihada zake mbalimbali za
kuwaletea maendeleo wananchi wa Nyakatuntu kwa kutekeleza miradi mbalimbali
katika Wilaya ya Kyerwa na tayari
imetenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa mradi wa barabara.
Kwa upande wake, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar
Zuber amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Majid Nsekela kwa
kuandaa dua hiyo kwa ajili ya baba yake na kusema kwa kufanya hivyo inaonesha
anaipenda familia yake nq dini yake ya kiislamu.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Majid Nsekela
amesema kuwa tukio hilo kwao ni la historia na wanamshukuru Mwenyezi Mungu kwa
neema hiyo.
“Kwa dua hii ya leo tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa Naibu
Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko pamoja na kuwa na kazi
nyingi amejumuika nasi hapa na wote mliopo nasi leo kwa upendo wenu na familia
yote imefurahi na inawashukuru,” amesema Bw. Nsekela.
Aidha, Bw. Majid amewakumbusha na kuwatakia heri wananchi wa Nyakatuntu kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu kwa kuchagua viongozi wanaofaa.
CHANZO: Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni