Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko
amewaasa Watanzania kuishi kwa kuvumiliana, kuheshimiana na kupendana kama
ilivyoagizwa na vitabu vya Mungu.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Septemba 15, 2024 katika
Kongamano la Tano la Ekaristi Takatifu Kitaifa lililofanyika katika Uwanja wa
Uhuru jijini Dar es Salaaam.
“Wote tuliokuja hapa tumesikia mahubiri mazuri, tumehubiriwa
kuwa wamoja zaidi tukavimiliane zaidi na
kuheshimiana kama Watanzania wamoja. Kuwa na mawazo tofauti kusitufanye tugawanyike Ekaristi Takatifu hii itufanye tuwe wamoja,” amesema Dkt.
Biteko.
Amesisitiza “Tuwafundishe jamii tuliyonayo kuwa na huruma
kwa watu wote wanaohitaji na muhimu zaidi kuwa na huruma na taifa letu la Tanzania.”
Akizungumzia kaulimbiu ya Kongamano hilo inayosema “Udugu
Kuponya Ulimwengu, Ninyi Nyote ni Ndugu”, Dkt. Biteko amesema kuwa kauli mbiu
hiyo ni muhimu na inawaunganisha watu pamoja.
Dkt. Biteko ameongeza “Tunapotoka hapa tuwafundishe watu,
tuwe wapya Ekaristi Takatifu imetuagiza tuishi upya.
Aidha, Dkt. Biteko amewahimiza Watanzania kushiriki katika
Uchaguzi Mkuu wa Serikali za Mitaa utakofanyika Novemba 27, 2024 kwa kuchagua
viongozi kulinga na sifa zao watakaosaidia kuleta maendeleo nchini.
Akihubiri katika misa takatifu wakati wa Kongamano hilo,
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Askofu Wolfgang Pisa,
amesema kuwa siku hiyo ni ya kuhitimisha Jubilei ya miaka 50 ya Jumuiya
Ndogondogo katika majimbo yote nchini.
Askofu Pisa amesema kuwa kwa miaka mingi nchini Jumuiya
Ndogondogo zimetumika kama chombo cha kuwafikia waumini wote na kuwa Ekaristi
Takatifu tu ndio kiunganisho cha wakristo.
“Hii ni sakramenti ya upendo hivyo tusibaguane kwa itikadi, rangi wala sababu zingine kwa kuwa sote tuna Mungu mmoja. Ndugu zangu twende katika sakramenti hii katika hali isiyo na dhambi, tumuombe Mungu sakramenti hii itubadilishe tuwe wapya,” amesisitiza Askofu Pisa.
Aidha, Askofu Pisa amewashukuru waamini wa kanisa hilo
kutoka majimbo mbalimbali nchini kwa kushiriki Kongamano hilo la Ekaristi
Takatifu na kusema kuwa baada ya kulihitimisha Kongamano hilo la tano
lilifofanyika kwa siku nne litakutana tena miaka minne ijayo katika Jimbo Kuu
la Arusha.
Akitoa salama za Baba Mtakatifu, Balozi wa Vatican nchini
Tanzania Askofu Mkuu Angelo Accattino amesema kuwa Kongamano hilo limeeleza
umuhimu wa Ekaristi Takatifu kama kiini cha imani yao.
“Ekaristi inatuunganisha na kristo na ndugu zetu katika
imani Ekaristi ina imarisha upendo wetu kwa Mungu. Naipongeza Serikali kwa
kufanya matukio kama haya kwa uhuru na amani,” amesema Askofu Accattino.
Kongamano hilo limekonga nyoyo za maelfu ya waumini wa
Kanisa Katoliki kutoka maeneno mbalimbali nchi nzima limehudhuriwa na mamia ya
viongozi wa dini wakiwemo maaskofu, mapadre na watawa.
Ambalo limehudhuriwa pia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. William Lukuvi, Waziri wa Ujenzi, Mhe.
Innocent Bashungwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Mhe. Albert Chalamila.
Viongozi wengine ni Spika wa Bunge Mstaafu, Anne Makinda, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Emannuel Nchimbi na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mhe. Tundu Lissu, Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika.
0 Maoni