Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imepongezwa kwa
kazi kubwa ya upandaji miti inayoendelea katika shamba la miti Silayo. Sambamba
na pongezi hizo watumishi wa shamba hilo wamekumbushwa kuwa wana wajibu mkubwa
wa kimkakati kupitia upandaji miti ili kuliwezesha taifa kukabiliana na athari
za mabadiliko ya tabia nchi zinazosababishwa na uharibifu wa mazingira.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.
Dunstan Kitandula alipokuwa akiongea na baadhi ya Viongozi na Askari wa hifadhi
ya Misitu wa Geita na Shamba la miti Silayo mkoani Geita ambapo Naibu Waziri
yupo mkoani Geita kufanya ziara ya kukagua maeneo ya misitu yaliyoathiriwa na
shughuli za kibinadamu.
Vilevile, Mhe.Kitandula alitumia fursa hiyo kuwakumbusha
Askari wa Jeshi la Uhifadhi kutimiza majukumbu yao kwa kuzingatia sheria,
taratibu na kanuni za utendaji kazi wao, na kutakiwa kujiepusha na vitendo vya
rushwa. "Timizeni majukumu yenu bila kuwaonea watu na muongozwe na hofu ya
Mungu; haifurahishi tunaposikia tuhuma mbalimbali zikielekezwa kwa askari wa
jeshi letu la uhifadhi wakati wa kutekeleza majukumu yenu" alisisiliza
Mhe. Kitandula.
Aidha Mhe. Kitandula alisema Askari wa Jeshi la Uhifadhi wa
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wanalo jukumu la msingi la kulinda na kuzuia mashamba na hifadhi za
misitu yasivamiwe wala kuharibiwa kwa shughuli za kibinadamu. Hivyo ishini
viapo vyenu vya utumishi mkikumbuka kuwa taifa linawategemea.
Vilevile Mhe. Kitandula alisema kuwa watumishi wa wakala wa
Huduma za Misitu Tanzania wanatakiwa kubadilika kimtazamo kwa kuacha kufikiria
moja ya chanzo kikubwa cha kuingiza mapato kwenye taasisi yao ni kutoa leseni
za kuchoma mkaa hivyo amewataka kufikiria ni namna gani mazao ya misitu
yanaweza kuchangia zaidi mapato. Alisema
bado ufugaji nyuki na mazao yatokanayo na asali unafursa kubwa ya kuwa chanzo
kikubwa cha mapato hivyo iwekwe mikakati madhubuti ya ufugaji nyuki na
kuzalisha asali yenye ubora kwa viwango vya kimataifa.
Kuhusu fedha za miradi ya huduma kwa jamii Mhe. Kitandula ameagiza kuwa fedha zote zinazotolewa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania zifuatiliwe kwa karibu na kufanya tathimini ili kujiridhisha kama miradi iliyofadhiliwa ina ubora unaolingana na thamani ya fedha zilizotolewa kutekeleza miradi hiyo.
Awali akimkaribisha katika Mkoa wa Geita Mhe. Martin
Shighella alimshukuru Naibu Waziri kufika katika Mkoa anaouongoza ili kujionea
changamoto ya uharibifu wa misitu katika hifadhi ya msitu wa Geita.
Mhe. Shighella alisema kuwa changamoto yauharibifu wa misitu katika mkoa wa Geita inachangiwa na shughuli za kibinadamu hasa uchimbaji wa madini unaoendelea katika mkoa huu kwa kuwa ndio shughuli kubwa ya kiuchumi kwa wananchi wa Mkoa wa Geita.
Na. Anangisye Mwateba- Katoro- Geita
0 Maoni