Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewahimiza wanawake nchini kutumia fursa ya mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa ajili ya kukopa na kujiongezea vipato.
Dkt. Biteko ametoa rai hiyo leo Septemba 14, 2024 mkoani
Singida wakati akimwalilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Kassim Majaliwa kwenye Kilele cha Maonesho ya Saba ya Mifuko na Programu za
Uwezeshaji kwa Mwaka 2024.
“Wanawake tumieni fursa iliyoweka na Serikali ya Mifuko ya
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ili muweze kukopa na kupata manufaa kutokana na
mikopo hiyo. Natoa wito kwa benki zote nchini muwaaamini wanawake kwenye mikopo
hii, mahali popote ukiona mwanamke anashughulika ujue faida inayopatika ni kwa
familia yote,” amesema Dkt. Biteko.
Dkt. Biteko amebainisha kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia alitoa
wito kwa benki kuongeza kiwango cha kutoa mikopo kwa wananchi huku akitolea
mfano Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ambayo mwaka 2020 ilitoa shilingi
bilioni 63 na hadi kufikia Agosti 2024 imetoa mikopo kiasi cha shilingi bilioni
337.
Ametaja takwimu za utoaji mikopo hiyo kutoka Benki ya TADB
kuwa wanaume ni asilimia 58.1, vijana asilimia 19 na wanawake asilimia 22.4
huku akisisitiza benki nchini kuendelea kuongeza kiwango cha utoaji mikopo kwa
wanawake.
“Mabenki endeleeni kuwaamini Watanzania, wakopesheni,
punguzeni masharti lakini wenye uwezo wa kulipa wapeni mikopo ili waweze
kufanyakazi,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Sambamba na hayo Dkt. Biteko amezindua Mwongozo wa Uratibu
na Usimamizi wa Mifuko na Programu za Uwezeshaji ili iwe nyenzo ya kuimarisha
utendaji wa mifuko na programu za uwezeshaji kwa lengo la kuondoa changamoto
zilizopo hasa mikopo chechefu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa katika kukuza
uchumi na kupunguza umaskini katika jamii.
Akizungumzia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Tanzania Bara utakaofanyika tarehe 27 Novemba 2024. Amewaasa wananchi wa Singida na Watanzania kuchagua viongozi kwa kuzingatia sifa zao na si dini, fedha wala ukabila.
“Ushiriki wenu katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
utawezesha kupata Viongozi wa Serikali za Mitaa ambao watachochea shughuli za
uchumi na kusimamia vyema miradi pamoja na mifuko na programu za uwezeshaji
zitakazokuwa zinaletwa katika maeneo yenu,” amesema Dkt. Biteko.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba
amesema kuwa Programu ya Uwezeshaji na elimu iliyotolewa mkoani Singida imegusa
akina mama wengi na uwezeshaji huo utabadilisha maisha ya wananchi wa mkoa huo.
“Programu za skimu za umwagiliaji zinalenga kupunguza
umaskini kwa mtu mmoja mmoja na uwezeshaji wananchi kiuchumi umeleta mabadiliko
makubwa mkoani kwetu,” amesema Dkt. Nchemba.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi,
Bi. Ben’g Issa amesema kuwa Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za
kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuwa na sera za kuwezesha wafanyabiashara
wadogo.
Ambapo imeanzisha mifuko na programu za uwezeshaji wananchi
kiuchumi na kutoa ruzuku katika sekta mbalimbali kwa kuwa bado wafanyabiashara
wadogo hawapati mikopo kwa urahisi.
“ Serikali imekuwa ikifanya maonesho ya mifuko na programu
za uwezeshaji ili kujenga uelewa kwa wananchi na kuonesha mifuko hii inavyoweza
kubadilisha maisha yao, pia imeendelea na vituo vya uwezeshaji wananchi
kiuchumi katika mikoa yote Tanzania Bara ili kuhakikisha huduma mbalimbali
ikiwemo mikopo, uongezaji thamani mazao, elimu ya kodi inawafikia wananchi,” amesema
Bi. Issa.
Aidha, amemshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha kwa ajili ya
kuimarisha programu ya Imarisha Uchumi na Mama Samia nchini inayolenga
kuhakikisha wananchi wote wanapata fursa za kushiriki katika shughuli za uchumi
na kukuza vipato vyao.
Maonesho ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji hayo yameongozwa kwa kaulimbiu inayosema “Shiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Unufaike na Fursa za Uwezeshaji".
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni