WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema marathon zinazofanyika
kila kona nchini ni mpango mkakati wa kuwafanya Watanzania wawe na afya njema
na wakae pamoja ili kubadilishana mawazo.
“Ni mkakati wa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwahamasisha wananchi wetu kufanya mazoezi ili kupunguza magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari na presha,” amesema Majaliwa.
Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumamosi, Septemba 14, 2024) wakati
akizungumza na viongozi na wadau mbalimbali walioshiriki Ruangwa Marathon 2024
(Msimu wa Pili) katika viwanja vya Madini, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
“Mbio hizi za Ruangwa ni zaidi ya mbio kwa sababu malengo
yake makubwa ni kuhamasisha wana-Ruangwa tuwe na umoja; tuimarishe ujenzi wa
afya zetu, tupate fursa ya kufahamiana na kuimarisha urafiki,” amesema Majaliwa.
Waziri Mkuu Majaliwa ambaye pia ni mbunge wa Ruangwa,
amewataka Wana-Ruangwa wajitokeze kusimamia miradi ya maendeleo iliyomo kwenye
wilaya hiyo na kupitia mkusanyiko mkubwa kama huo watengeneze mijadala ya
kiuchumi katika ngazi na makundi tofauti waliyopo.
Amewashukuru washiriki wa mbio hizo za km.21, km.10, km.5 na
km.3 kwa watoto kutoka Ruangwa na wilaya za jirani za Nachingwea na Liwale
lakini pia vikundi vya hamasa na marathon kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Iringa
na Mtwara.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel
alisema watu wanashauriwa kufanya mazoezi ili kupunguza magonjwa yasiyoambukiza
na endapo watafuata hayo maelekezo, Serikali itaokoa fedha nyingi zinazotumika
kutibu magonjwa hayo.
“Nchi yetu inapoteza sh. bilioni 454 kwa mwaka kwa kutibu
watu wenye magonjwa ambayo tukifanya mazoezi tu, nchi yetu inakuwa salama.
Fedha hizi zingetumika kujenga shule za msingi mpya 1,513 zenye madarasa nane
na ofisi za walimu,” alisema Dkt. Mollel.
Mapema, Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Hamis
Mwinjuma alisema Ruangwa Marathon inaelekea kuwa ya Kimataifa katika miaka
michache ijayo. Alimpongeza Mbunge wa Ruangwa kwa kuandaa marathon hiyo ikiwa
ni utekelezaji wa maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Naye, msanii wa Bongo Fleva nchini, Naseeb Abdul maarufu
kama Diamond Platnumz ametoa pongezi kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
kujenga miradi ya maendeleo wilayani Ruangwa ikiwemo barabara ya lami ya kutoka
Nanganga.
“Mwaka jana tulikuja kufanya tamasha na njia nzima ilikuwa rough sana, nikawa najiuliza kama tungeweza kurudi salama tulikotoka. Lakini mwaka huu, nimeshangaa sana. Tumekuja kwenye lami tangu njiapanda. Leo hapa Ruangwa, tutazindua tamasha la mwaka huu la Wasafi Festival na kisha tutaendelea na mikoa mingine,” alisema.
0 Maoni