Naibu Katibu
Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Utalii, Nkoba Mabula,
amepongeza mchango mkubwa wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika
kukuza utalii ikolojia na kuimarisha juhudi za uhifadhi wa mazingira nchini.
Akizungumza
wakati wa ziara yake kwenye maeneo yanayosimamiwa na TFS jijini Tanga aliyoifanya
jana, Mabula alisisitiza umuhimu wa utalii endelevu katika kuchochea maendeleo
ya kiuchumi huku ukiendelea kulinda mazingira.
Mabula
alieleza kuwa utalii wa misitu ni moja ya nyenzo muhimu za kuongeza mapato kwa
jamii za ndani na wakati huohuo kuhamasisha uwajibikaji miongoni mwa wakazi.
"Utalii ikolojia hauleti tu faida kwa
jamii, bali pia unasaidia katika kuwafanya watu wa maeneo haya kutambua umuhimu
wa kuhifadhi rasilimali zao za asili," alibainisha Mabula.
Aliongeza
kuwa TFS imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha misitu inatumika kwa njia
endelevu ili kunufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.
"Kwa
mfano, leo nimetembelea na kujionea misitu ya mikoko, magofu ya Tongoni, na
Shamba la Miti Longuza, hakika kuona ni kuamini, misitu pekeyake ni kivutio
tosha cha utalii. Maeneo haya ya mashamba na misitu yanaweza kuimarishwa kwa
kuboresha miundombinu ya utalii na kutengeneza mikakati ya masoko kukuza
shughuli za utalii," alisema.
Alisisitiza
kuwa uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na TFS, hasa kwenye mikoko iliyopo
pembezoni mwa Hoteli ya Tanga Beach, Tongoni na Shamba la Miti Longuza mkoani
Tanga, unahitaji kuambatana na hadithi zenye kuvutia zinazoweza kutangaza
utalii wa misitu na malikale, huku zikiweka bayana umuhimu wa kulinda mifumo ya
ikolojia.
Akieleza
zaidi, Mabula alisisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa jamii katika usimamizi
wa misitu kwa matokeo bora ya uhifadhi. "Wakati jamii zinapoona manufaa
halisi kutoka kwa utalii, kuna uwezekano mkubwa wa kushiriki katika mazoea
endelevu na kulinda mazingira yao," alieleza.
Kwa
kumalizia, Mabula alitoa wito wa ushirikiano kati ya TFS, jamii za ndani, na
serikali ili kuendeleza mkakati wa kina wa utalii unaopendelea ukuaji wa
kiuchumi na uendelevu wa mazingira. "Kwa pamoja, tunaweza kuhakikisha kuwa
misitu ya Tanzania inabaki kuwa chanzo cha fahari na ustawi kwa vizazi
vijavyo," alihitimisha.
Kamanda wa
Uhifadhi Kanda ya Kaskazini, James Nshare, alimshukuru kwa niaba ya Kamishna wa
Uhifadhi wa TFS na kueleza kuwa maelekezo yote yaliyotolewa yamepokelewa na
yatafanyiwa kazi.
Aliahidi pia
kuimarisha ushirikiano kati ya ofisi zote za TFS na wadau mbalimbali katika
kukabiliana na changamoto za uhifadhi, hususan moto, ambao ni moja ya
changamoto kuu katika mashamba na misitu ya hifadhi.
“Wenzetu
kwenye Halmashauri wana sheria ndogo za kuzuia moto kuanzishwa ndani ya misitu,
pia sheria yetu ya misitu inawataka watu kushiriki kuzima moto unapotokea!
Hivyo, ni muhimu tushirikiane katika kukabiliana na majanga ya moto,” anasema.
Na. Tulizo
Kilaga- Tanga
0 Maoni