Wilaya ya
Lushoto mkoani Tanga imeandika historia mpya kwa kuzindua rasmi tamasha lake la
kwanza la Utalii linalolenga kuunga mkono juhudi za Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan katika kukuza sekta ya utalii nchini.
Akizungumza
muda mfupi kabla ya uzinduzi huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na
Utalii (anayeshughulikia Utalii), Nkoba Mabula, alisisitiza umuhimu wa tamasha
hili katika mkakati wa kuimarisha utalii.
"Tamasha
hili lililobeba kauli mbiu "ALIANZISHA MAMA SISI TUNAENDELEZA" ni
sehemu ya juhudi za kukuza utalii, kuvutia wawekezaji, na kutoa huduma bora kwa
watalii," anasema.
Mabula
alieleza kuwa lengo ni kuongeza idadi ya watalii kufikia milioni tano na mapato
ya utalii kufikia dola za Marekani bilioni sita.
Aliongeza
kuwa ushirikiano wa kila mmoja ni muhimu ili kufanikisha malengo hayo, hasa
katika kutoa huduma bora kwa watalii ili kuwahamasisha kurudi tena lakini pia
kuboresha miundombinu ili kuendeleza uhifadhi.
Aidha, kwa
niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Pindi Chana, Mabula
aliipongeza mkoa wa Tanga kwa kuandaa matamasha ya mara kwa mara, akibainisha
kuwa hayo ni hatua muhimu katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi.
"Matamasha
kama haya yana mchango mkubwa katika kufikia malengo ya kukuza utalii na ni
mfano wa kuigwa na mikoa mingine, kwa niaba ya wizara, niendelee kutoa rai kwa
viongozi wenzangu tuendelee kutumia matukio mbalimbali wananchi kutembelea
vivutio vya utalii ili kukuza utalii wa ndani," alisisitiza.
Mabula pia
alihitimisha kwa kuwataka viongozi na wadau mbalimbali wanaotoa huduma katika
mnyororo wa thamani wa sekta ya utalii kuhakikisha wanaendelea kutoa huduma
bora ili watalii wanotembelea vivutio hivyo washawishike kurudi na kuvitangaza
kwa ndugu na jamaa zao.
Aliongeza
kuwa, Mhe. Rais alielekeza wadau wote wa utalii kushirikiana ili kuyaendeleza
matukio ya namna hiyo katika kutangaza utalii na biashara na hivyo kutoa rai
kwa mikoa na halamashauri nchini kuendelea kushirikiana na wadau wa utalii
katika kubuni matukio ya utangazaji wa utalii, na kusisitiza Wizara yake kutoa
ushirikiano wakutosha.
“Kupitia
Mhe. Rais sasa hivi ipo fedha imetengwa mahususi kwaajili ya kuendeleza sekta
ya utalii katika maeneo mbalimbali ikiwemo ya mikoa na wilaya, ni juhudi yetu
sisi kuhakikisha kwamba vivutio vya utalii vilivyopo katika maeneo yetu
vinatambulika na Wizara, ivione na viweze kuelezeka kwa ufasaha kwaajili ya
kuvitangaza,” anasema.
Awali, Mkuu
wa Mkoa wa Tanga, Mheshimiwa Balozi Dkt. Batilda Salha Burian, alielezea
umuhimu wa utalii katika uchumi wa Tanzania, akisisitiza kuwa tamasha hilo
linatoa fursa ya kipekee ya kuonyesha vivutio vya utalii vya Mkoa wa Tanga,
kama vile Hifadhi ya Taifa ya Saadani na Milima ya Usambara.
Aliipongeza
Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kwa maandalizi mazuri na kutoa rai kwa
Halmashauri nyingine kuiga mfano huo.
Dkt. Burian
pia aliwasihi wananchi kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vya ndani ili
kusaidia kukuza uchumi wa taifa. “Kutembelea vivutio vyetu ni hatua muhimu ya
kukuza utalii wa ndani na kuimarisha uchumi wa taifa,” alisema, akibainisha
kuwa idadi ya watalii inaongezeka kila mwaka na mwaka huu pekee inatarajiwa
kufikia zaidi ya watalii 105,230.
Katika hafla
hiyo, Dkt. Burian alizindua Jengo la Utalii (Tourism Information Center) pamoja
na Mpango Kazi wa Utalii, huku akiwahimiza wadau wote kutoa taarifa sahihi
kuhusu vivutio vya utalii ili kuvutia wageni zaidi.
Tamasha la
Utalii Lushoto, ambalo linaonesha utamaduni, michezo, na burudani mbalimbali,
linatarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya sekta ya utalii na
uchumi wa Mkoa wa Tanga. Aidha, tamasha hili linalenga kutoa fursa kwa wageni
wa ndani na nje kuona vivutio vya utalii vya Lushoto na kuhamasisha wananchi
kuendelea kuwekeza katika sekta hii muhimu.
0 Maoni