Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Maafisa waandamizi wa
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na viongozi wa vyombo vya usalama wa Wizara
hiyo kutekeleza kwa vitendo na kuiishi falsafa ya R nne (4R) ya Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Amesema kuwa ni muhimu kuifahamu vyema falsafa hiyo ya Rais
Dkt. Samia na kuitekeleza kwa vitendo. “Nina imani kubwa kwamba uongozi wa juu
wa Wizara umeielewa vizuri falsafa hiyo, na semina hii elekezi ni ushahidi
tosha wa kuitekeleza kwa vitendo”
Amesema hayo jana Ijumaa, Septemba 06, 2024 wakati
alipofungua Semina elekezi kwa viongozi waandamizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani
ya Nchi iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Weruweru River
Lodge, mkoani Kilimanjaro.
“Falsafa hii inajikita katika masuala ya Maridhiano
(Reconciliation), Ustahamilivu (Resilience), Mageuzi (Reforms), na Kujenga upya
Taifa (Rebuilding). Hivyo, nitoe wito kwa washiriki ambao ni Maafisa Waandamizi
wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
pamoja na Menejimenti ya Wizara na Taasisi zake kuendelea kushiriki na kuishi
kikamilifu falsafa hii”
Ameongeza kuwa semina elekezi hiyo ni sehemu muhimu kwa
maendeleo ya kitaaluma na kitaasisi kwa maafisa waandamizi wa vyombo vya
usalama, na husaidia katika kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi
na kwa kufuata viwango vya kitaaluma na kisheria.
“Semina elekezi hutoa fursa kwa maafisa waandamizi kujifunza
mbinu na taratibu mpya katika utendaji wa majukumu yao. Hii inajumuisha
teknolojia mpya, mbinu bora za ulinzi na usalama, na mbinu za kisasa za
kupambana na uhalifu.”
Kwa Upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi
Hamad Masauni amemshukuru Rais Dkt. Samia juu ya nia yake ya dhati kwa kufanya
maboresho ya Wizara hiyo na vyombo vyake ikiwemo Jeshi la Polisi, Magereza,
Uhamiaji na Zimamoto pamoja na Taasisi ya NIDA.
“Maboresho haya yanahusisha upandishaji vyeo wa kihistoria
wa Maafisa, Wakaguzi na Askari wapatao 50,971, kuongeza Bajeti ya Miradi ya
Maendeleo kutoka mwaka 2021/22 hadi 2024/25 ni Shilingi 262.2 ambayo ni sawa na
asilimia 954.59 ya ongezeko la Bajeti ya Miradi ya Maendeleo”
Amesema kuwa Ongezeko hilo la bajeti limesaidia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa vitendea kazi ikiwemo magari, mitambo, boti, vifaa vya TEHAMA na kadhalika.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni