Basi lagonga gema na kuua watu 12 akiwamo dereva

 

Basi la abiria la kampuni ya AN Classic likitokea Mbeya kuelekea Tabora kupitia Wilaya ya Chunya limepata ajali kusababisha vifo watu 12 akiwamo dereva wa basi hilo, huku majeru 33 wakipelekwa hospitali.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa mkoa huo ACP Wilbert Mica Siwa ajali hiyo imetokea jana majira ya saa 1:30 asubuhi huko katika eneo la Lwanjilo, Wilaya ya Mbeya katika barabara ya Mbeya baada ya basi kuacha njia na kwenda kugonga gema na kisha kupinduka.

ACP Siwa amesema Katika ajali hiyo watu 12 wamepoteza maisha kati yao wanaume 5 akiwemo aliyekuwa Dereva wa Basi hilo Hamduni Nassoro Salum, wanawake 7 miongoni mwao watoto wadogo 2.

Aidha, katika ajali hiyo watu 33 ni majeruhi ambao kati yao 22 ni wanaume na 11 ni wanawake. Majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Hospitali ya Wilaya ya Chunya na Kituo cha Afya Chalangwa kilichopo Wilaya ya Chunya.

Kamanda Siwa amesema uchunguzi wa awali uliofanywa umebaini kuwa chanzo cha ajali ni uzembe wa Dereva kushindwa kulimudu gari lake kwenye eneo lenye mteremko na kona kali.

Jeshi la Polisi linaendelea kutoa wito kwa madereva kuwa makini na kuzingatia sheria, alama na michoro ya usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.

Chapisha Maoni

0 Maoni