Mhe. Abdou aliyasema hayo jana Septemba 1, 2024 baada ya
kutembelea vivutio adhimu vya utalii katika Hifadhi hiyo ambapo amesema kwamba
amefurahishwa sana na wanyama kwani akiwa nchini kwake amekuwa akiwaona wanyama
hao kwenye sinema pekee.
“Leo hii nimefika katika Hifadhi ya Taifa Mikumi kwa ajili
ya utalii,nimefurahishwa sana na wanyama ambao nimebahatika kuwaona napenda
kuuhakikishia uongozi wa Hifadhi hii na Serikali ya Tanzania kwa ujumla kwamba
nikirudi kwetu Comoro nitakuwa balozi wa kutangaza vivutio nilivyoviona,” alisema Abdou.
Mhe. Abdou pia, aliupongeza uongozi wa Hifadhi hiyo kwa
kuhakikisha wanyama wote wanalindwa na kutunzwa dhidi ya wahalifu wakiwemo
majangili ambapo alieleza kuwa kitendo cha kuwalinda wanyama hao Tanzania
inanufaika zaidi kiuchumi kutokana na mapato yatokanayo na utalii.
Aidha, alitoa wito kwa jamii kufichua vitendo viovu vya
ujangili na kuwasa wanaojihusisha na vitendo hivyo vya ujangili kuachana na
tabia hiyo kwani vivutio ambavyo ameviona hususani wanyamapori kama vile Tembo,
Nyani, Pundamilia, Swala, Viboko, Mamba na wengine wengi ni kwa sababu wanyama
hao wanalindwa na kutunzwa vizuri.
“Nchi ya Comoro pamoja na Tanzania ni ndugu, tumekuwa
marafiki wa muda mrefu na tumekuwa tukishirikiana katika masuala mbalimbali kwa
maslahi mapana ya nchi hizi zote, hivyo na mimi pia nawaalika Watanzania kuja
Comoro kutalii kwani ni nchi ya visiwa vingi hivyo mtajifunza kuogelea na
kufuga samaki,” alisema Mhe. Abdou.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje Ulinzi
na Usalama, Mhe. Vita Kawawa (Mb) alisema anaushukuru uongozi wa Hifadhi hiyo kwani
umeonesha ukarimu wa hali ya juu kwa Spika huyo ambapo anaamini ukarimu huo
unatokana na misingi imara iliyojengwa na waasisi wa Taifa letu Tanzania.
Mhe. Kawawa alisema kuwa ziara ya Spika huyo katika hifadhi
hiyo kutafungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwani wananchi wengi wa Comoro
watahamasika kwa wingi kuja kutalii katika hifadhi zilizopo hapa nchini hali
ambayo itadumisha ushirikiano uliopo katika masuala ya kidiplomasia na
kibiashara.
Kwa upande wake, Afisa Uhifadhi Mkuu, David Kadomo kwa niaba ya Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mikumi, alisema uongozi wa hifadhi hiyo kwa kipekee kabisa una kila sababu ya kushukuru kupata ugeni huo mkubwa ambapo alisema kitendo cha Spika huyo kutembelea Hifadhi ya Taifa Mikumi utafungua fursa kwa wananchi wengine wa Taifa hilo kuja Tanzania kutalii.
Na Zainab Ally- Mikumi
0 Maoni