Rais wa Jamuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya kikazi katika Jamhuri ya Watu wa China kuanzia tarehe 02 hadi 06 Septemba, 2024 kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (Forum on China-Africa Cooperation-FOCAC) utakaofanyika jijini Beijing.
Aidha, wakati wa ziara hiyo Rais Dkt. Samia atakutana na
mwenyeji wake Mhe. Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China kwa mazungumzo
yanayolenga kuimarisha uhusiano muri na wa kihistoria kati ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China ulioasisiwa miaka 60
iliyopita.
Marais hao wawili pamoja na Rais wa Jamhuri ya Zambia, Mhe.
Hakainde Hichilema watashiriki na kushuhudia uwekaji saini wa Hati za
Makubaliano ya Uboreshaji wa Reli ya TAZARA.
Pamoja na mambo mengine, miongoni mwa maeneo yanayotarajiwa
kupewa kipaumbele kwenye Mkutano wa FOCAC ni uendelezaji wa miundombinu, kukuza
uwekezaji, uendelezaji wa viwanda, kilimo cha kisasa na amani na usalama.
Rais Dkt. Samia anatarajia kuwa miongoni mwa Wakuu wa Nchi
watakaohutubia funguzi wa Mkutano wa FOCAC akizungumza kwa niaba ya Kanda ya
Afrika Mashariki.
Pembezoni mwa mkutano huo, katika kukuza biashara na uwekezaji, Rais Dkt. Samia atakutana na makampuni na wawekezaji kutoka Jamhuri ya Watu wa China kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji zaidi chini Tanzania.
0 Maoni