Tume yatangaza ratiba ya Uchaguzi Mdogo wa Ubunge Chamwino na Udiwani Kata 11

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza Novemba 04, 2026 kuwa siku ya uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Chamwino, Mkoa wa Dodoma, pamoja na Madiwani katika kata 11 za Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume, Ramadhani Kailima, imesema uchaguzi huo unafanyika kufuatia kuwepo kwa nafasi wazi za uongozi katika maeneo ya uchaguzi.

“Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ilipokea taarifa kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu kuwepo kwa nafasi wazi ya Ubunge katika Jimbo la Chamwino, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Mkoa wa Dodoma,” ilisema taarifa hiyo.

Nafasi hiyo imetokea baada ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Deogratius John Ndejembi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Uteuzi wake ulifanyika tarehe 26 Agosti, 2026 na kuthibitishwa na Bunge tarehe 28 Agosti, 2026.

Aidha, Kailima kupitia taarifa hiyo amesema Tume kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 57(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Sura ya 343 ilipokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana juu ya uwepo wa nafasi wazi za madiwani 11 kwa Tanzania bara.

“Tumepokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa kuhusu uwepo wa nafasi wazi za madiwani 11 kwa Tanzania Bara. Nafasi hizo wazi zilitokana na vifo vya madiwani nane (08) kwa nyakati tofauti na madiwani watatu (03) kujiuzulu,”taarifa ilisema.

Tume imesema kuwa fomu za uteuzi kwa wagombea wa Ubunge Chamwino na Udiwani katika kata 11 zitatolewa kuanzia tarehe 7 hadi 13 Oktoba 2026, huku zoezi la uteuzi wa wagombea likifanyika tarehe 13 Oktoba 2026.

Baada ya uteuzi, kampeni za uchaguzi zitaanza tarehe 14 Oktoba 2026 na kuendelea hadi 3 Novemba 2026.

Kailima amesema Uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Chamwino na Madiwani katika kata 11 za Tanzania Bara utafanyika siku ya Jumatano tarehe 04 Novemba, 2026.

Kailima amezitaja Kata 11 zitakazofanya uchaguzi Uchaguzi wa Madiwani kuwa ni Nonde – Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Lugenge – Halmashauri ya Mji Njombe, Bargish – Halmashauri ya Mji Mbulu, Makole – Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Mwera – Halmashauri ya Wilaya ya Pangani na Oldonyosambu – Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.

Kata zingine ni pamoja na Igalula – Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, Shelui – Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Mvumi – Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Nyarero – Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Ilolangulu – Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe.

Tume imevikumbusha vyama vya siasa, wagombea na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia Katiba, sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, taratibu, miongozo na maelekezo ya Tume katika kipindi chote cha utekelezaji wa ratiba hiyo.

 

Chapisha Maoni

0 Maoni