Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Biteko
amesema Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria
kuipatia Kigoma miradi ya maendeleo na fursa mbalimbali ili kuufungua mkoa huo
kiuchumi.
Akihutubia katika mkutano wa hadhara katika Kata ya Kasanda
Wilaya ya Kakonko leo Septemba 18, 2024 Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali
imetekeleza miradi mingi ya maendeleo mfano hospitali na barabara
ikilinganishwa na kipindi kilichopita ambapo wananchi walikuwa kitaabika kupata
huduma mbalimbali za kijamii.
“ Halmashauri hii imeanzishwa mwaka 2013 na kwa kiasi
kikubwa maeneo mengi yalikuwa mapori lakini leo tumetembelea Hospitali ya
Wilaya ya Kakonko hali halisi ya maendeleo inaonekana. Rais wetu anataka Kigoma
ifikike na watu wakae kwa amani na kufurahia kuwa Kigoma, nimefurahi sana kuona
majengo ya hospitali ya wilaya,” amesema Dkt. Biteko.
Awali wananchi wa Kakonko walikuwa wakipata huduma za afya
kutoka Hospitali ya Bugando na Geita, uwepo wa hospitali hiyo utasaidia
kupunguza gharama ya kufuata mbali huduma za afya.
Akizungumzia barabara ya Kakonko hadi katika mpaka wa
Tanzania na Burundi Dkt. Biteko amesema maisha ya watu ni kipaumbele kwa
Serikali ya Awamu ya Sita. "Hatutaki maigizo kwenye maisha ya watu,
tunataka kuwahakikishia hata barabara ya Nyakanazi Kasulu hadi Kigoma
inaunganishwa kwa lami. Rais Samia anataka kuona tunafanya biashara na majirani
zetu na kuwa mpakani sio laana bali ni fursa na milango ya biashara
itafunguliwa na barabara hii yenye urefu wa km 48 ya Kakonko hadi mpakani
itasimamiwa na TANROADS,” amesema Dkt. Biteko.
Vilevile, amewapongeza wananchi wa Kakonko kwa kuzalisha
chakula cha ziada tani 81,000 ambapo mahitaji ni tani 76,000 na tani za chakula
zilizopo ni tani 157,000.
Fauka ya hayo, Dkt. Biteko ametoa wito kwa viongozi wa Chama
cha Mapinduzi (CCM) kuendesha mchakato mzuri wa kura za maoni na wachague
wagombea wenye sifa na sio kutumia rushwa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Zainabu Katimba amesema kuwa Rais Samia
amefanya uwekezaji wa zaidi ya shilingi bilioni
4 kwa ajili ya majengo na vifaa tiba katika Hospitali ya Wilaya ya
Kakonko, aidha ametoa maelekezo mahsusi kuwa hospitali zote za wilaya nchini ziwe na wodi ya watoto ili kupunguza vifo kwa
mama na mtoto.
Vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka 556 hadi 104
katika vizazi hai 100,000. Mhe. Katimba
amesema hayo mafanikio hayo ni matokeo ya jitihada kubwa inayofanywa na
Rais Samia kwa ajili ya akina mama nchini.
Pia, Mhe. Katimba amezungumzia barabara na kusema kuwa awali wilaya hiyo ilikuwa inapokea kiasi cha
shilingi milioni 700, katika kipindi cha
Rais Samia ameongeza fedha hadi kufikia shilingi bilioni 2.2 kwa ajili ya
barabara za dharura.
“ Barabara inayoelekea hospitali ya wilaya yenye urefu wa km
1, mwaka huu Mhe. Rais ametoa fedha
shilingi milioni 450 ili iweze kujengwa na muweze kufika hospitali vizuri,
hakika wilaya hii imepata uwekezaji mkubwa,” amebainisha Mhe. Katimba.
Aidha, amewahimiza wananchi wa Kakonko kujiandikisha katika daftari
la wapiga kura na baadae kushiriki
katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024.
Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kakonko na Diwani Kata ya
Gwarama, Bw. Fidelis Nderego amesema “ Kakonko tukipata barabara ya kiwango cha
lami hadi Soko Kuu la ujirani mwema kati ya Kakonko na Burundi uchumi wa
wananchi wa Kakonko na Mkoa wa Kigoma utafunguka kiuchumi.”
Aidha, mkazi wa Kakonko, Maita Paschal amesema kuwa uwepo wa
Hospitali hiyo ya Wilaya ya Kakonko unawasaidia wananchi kupata huduma karibu
kuliko ilivyokuwa awali ambapo walisafiri umbali mrefu kupata huduma.
Huduma sasa ni nzuri na zipo karibu na nyumbani, awali nilijifungua watoto wangu kumi hospitali ya mbali Mgaza lakini sasa tunapata huduma karibu na nimekuja kumuona mwanangu ambaye amejifungua hapa,”amesema Maita.
0 Maoni