Daktari Bingwa Mbobezi wa Upasuaji Ubongo Mgongo na Mishipa
ya Fahamu Prof. Huh Seung Kon kutoka Korea Kusini ameupongeza uongozi wa
Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa mageuzi na maboresho makubwa
iliyofanya katika kuendelea kuberesha utoaji wa huduma za afya nchini.
Prof. Huh ametoa pongezi hizo alipotembelea hospitali hiyo
kwa lengo la kukutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa hospitali pamoja
wataalam wanaofanya kazi katika Idara ya Upasuaji Ubongo, Mgongo na Mishipa ya
Fahamu idara ambayo amehuduma kwa kipindi cha takribani miaka minne kabla ya
kurejea nchini Korea mwaka 2022.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mtendaji MNH-Mloganzila
Dkt. Julieth Magandi amemshukuru Prof. Huh kwa ujio wake kwani unaendelea
kuongeza chachu katika kutoa huduma za ubingwa bobezi katika hospitali hiyo kwa
manufaa ya Watanzania.
Dkt. Magandi ameongeza kuwa Muhimbili-Mloganzila imeendelea
kunufaika na Prof. Huh na kutoa mfano kuwa wauguzi watatu walienda kupata
mafunzo ya muda mfupi nchini Korea na wengine watatu wapo nchini Korea kwa
mafunzo kwa ufadhili wa daktari huyo.
Prof. Huh alikuja nchini kwa mara ya kwanza mwaka Disemba mwaka 2019 na kuondoka nchini mwaka 2022 ambapo katika kipindi hicho aliwajengea uwezo wataalam wa Idara ya Upasuaji Ubongo Mgongo na Mishipa ya Fahamu na walifanikiwa kuanzisha huduma ya ubingwa bobezi kwa kutumia njia ya kisasa ya upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye sakafu ya ubongo kwa kutumia matundu ya pua.
0 Maoni